Smart Darasa kutatua changamoto masomo ya sayansi

DAR ES SALAAM; CHANGAMOTO ya kutokuwepo maabara za sayansi zenye vifaa vya kutosha kwa ajili ya kufanya mazoezi ya kisayansi kwa vitendo katika baadhi ya shule za msingi na sekondari Inachangia kutofanya vizuri kwa wanafunzi.

Ingawa serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha shule zake pamoja na miundombinu iliyopo ili kuinua kiwango cha ufaulu, Changamoto ya vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa upande wa maabara kwa masomo ya sayansi zimeendelea kuathiri uelewa, ufaulu na mapenzi ya wanafunzi kwenye masomo hayo, yakiwemo Fizikia, Kemia na Baiolojia.

Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), imekuwa ikiratibu sayansi, teknolojia na ubunifu ikiwa ni pamoja na kutoa ufadhili kwa teknolojia, ubunifu na tafiti zinazofanya vizuri kwa lengo la kuwezesha kuleta matokeo chanya kwa jamii.

Hivyo basi ubunifu wa kidijitali umefanywa ili kuwezesha kutatua changamoto ya elimu kwa kuwa wanafunzi na walimu wataweza kujifunza na kufundisha kwa kutumia teknolojia.

Kusiluka Aginiwe ni Mkurugenzi wa Mikakati katika kampuni ya Smart Darasa iliyojikita kutatua changamoto ya elimu kwa kujifunza masomo ya sayansi kwa vitendo kuwa ni rahisi kwa kutumia vifaa vya kidijitali.

Mfano hai wa teknolojia hii unatolewa na Mwalimu wa Nidhamu na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa Shule ya Sekondari Dovya iliyoko Chamazi, Samson Mfungaro kwa kusema kuwa shule hiyo ina miaka mitatu sas,a lakini haina maabara, hivyo wanatumia teknolojia hiyo ya Smart Darasa kufundishia wanafunzi.

“Kwetu sisi teknolojia hii imekuwa ni mkombozi. Kwa kuwa wanafunzi wanafurahia masomo ya sayansi na kuyapenda,” anasema.

 

Akielezea kuhusu shule hiyo, Aginiwe anasema walifanikiwa kutoa semina katika shule hiyo, na kupata ushuhuda kutoka kwa baadhi ya walimu, mzazi mmoja ambaye ni mhandisi kuwa alimtoa mtoto wake kwa kuwa shule hiyo haina maabara.

“Katika Shule ya Chamazi kuna mzazi mmoja ambaye ni mhandisi hii tulipata kutoka kwa walimu baada ya kwenda pale kufanya mafunzo mwezi wa saba mwaka jana, tukapewa ushuhuda wa tukio lililotokea mwezi wa sita.

“Shule ile haina maabara mzazi ni mhandisi alimtoa mwanafunzi wake kutoka kwenye ile shule kwa sababu aliwaambia walimu pale hawamtengenezi mtoto wake kuwa mhandisi kwa sababu shule haina maabara, wanajifunza mambo kwa picha zaidi.

“Wale walimu wakasema hii Smart Darasa ingekuwepo mwezi mmoja kabla tunatumai yule mzazi angemwacha mwanafunzi wake ndani ya shule yetu kwa sababu angeweza kujifunza kwa vitendo na kwa namna ya kidijitali, angeweza kujifunza hata akiwa nyumbani kwa hiyo huo ni mfano mdogo wa kuonesha kuwa wazazi wangependa watoto wao waweze kujifunza kwa vitendo siyo kwa nadharia peke yake,” anasema.

Mkurugenzi wa Mikakati katika kampuni ya Smart Darasa, Kusiluka Aginiwe

Japokuwa shule hiyo haina maabara, Aginiwe anasema serikali imefanya hatua kubwa kwenye mageuzi ya kidijitali kwa maana imeweza kusambaza vishikwambi kwa walimu wote katika shule zote za serikali nchini, jambo ambalo ni hatua kubwa sana kwa teknolojia ya Smart Darasa.

Maana yake ni kwamba, mwalimu akiwa popote Tanzania ataweza kufundisha kwa vitendo akiwa darasani hata kwa kutumia kishikwambi chake anaweza akakaa na magrupu ya wanafunzi akielekeza ujumbe fulani kidijitali zaidi.

Kwenye shule hiyo baada ya kuwapa mafunzo ya jinsi ya kuitumia teknolojia hiyo, sasa wanatumia Smart Darasa kama maabara ya kidijitali.

Japokuwa shule hiyo haina maabara, kwa kutumia teknolojia hiyo ya Smart Darasa imeweza kufaulisha wanafunzi wa kidato cha pili, sasa hivi wanaelekea kwenda hatua ya kidato cha nne.

“Kwa hiyo hilo ni somo dogo ama jinsi ambavyo Smart Darasa inaweza kusaidia hizi jamii ambazo hazijafikiwa kwa ukubwa huo, tunaamini kazi ya serikali ni kubwa na matatizo ya nchi hii ni mengi nasi tunajitahidi kusaidia serikali kwa upande huo kujifunza au kufundisha kwa vitendo,” anasema.

Anasema utumiaji wa teknolojia hiyo ni kuchangia kubadilisha matokeo ya wanafunzi wanaopata alama D na F katika masomo ya Fizikia, Kemia, Bbailojia na Hisabati.

“Sasa tukafikiria kuwa, kujenga maabara zinahitajika zaidi ya shilingi milioni 20. Lakini kwa kutumia maabara za kidijitali tunaweza tukawafikia watu wengi zaidi popote Tanzania kwa gharama ndogo zaidi kwa hiyo mtu anaweza kufanya majaribio yale yale anayofanya katika maabara ya shuleni akaifanya ya kidijitali kwa kutumia Smart Darasa na akaelewa anachotakiwa kufanya,” anasema.

Anasema kupitia teknolojia hiyo wanataka kubadili mtazamo kuwa masomo ya sayansi ni ya wanaume ama ni wale wanatokea familia ya vigogo ndio wanaweza kujifunza kiurahisi.

Maelezo yake ni kwamba Smart Darasa ipo kwa ajili ya wanafunzi na walimu, kwa maana wanafunzi wanatafuta njia rahisi ya kujifunza masomo ya sayansi na kuyaelewa ndio maana wanaenda kwenye masomo ya ziada maarufu kama twisheni.

Walimu nao wana wakati mgumu wa kufundisha masomo ya sayansi kwa maana kwamba inabidi wayafundishe wakiwa na vifaa mbalimbali vya kuelezea kwa vitendo darasani, sasa hii inahitaji muda mwingi na fedha nyingi.

Teknolojia hiyo inamsaidia mwalimu kuandaa vifaa vya kufundishia kwa vitendo kuonesha majaribio yanafanyikaje, hivyo tangu wameianzisha teknolojia hiyo mwitikio umekuwa ni mzuri kutoka kwa wanafunzi na walimu hali iliyowapa moyo wa kuendelea kupambana.

“Kwa msaada mkubwa na ufadhili wa Costech tumeweza kufikia watu wengi kupitia maonesho ya Sabasaba, Makisatu na mengine ambayo tunaenda chini ya mwavuli wa Costech .tumeweza kutengeneza maudhui zaidi kwa ajili ya kuwaonesha Watanzania.

“Kifupi hatujajitangaza kwa hela yoyote lakini tumeweza kupata watumiaji wa simu za android zaidi ya 2000, watumiaji wa website zaidi ya 10,000 na tunategemea tukimaliza maudhui tutaweza kuwafikia watu wengi zaidi,” anasema.

Mkurugenzi wa Mikakati katika kampuni ya Smart Darasa, Kusiluka Aginiwe, akionesha teknolojia hiyo inavyofanya kazi

Anasema Costech imewawezesha kupata zaidi ya Sh milioni 70 za Kitanzania ambazo kwa kushirikiana na wadau wengine wamefanikisha kufikia hapo walipo.

Anaeleza kuwa mbali na Tanzania, teknolojia hiyo inatumiwa na nchi za Kenya, Nigeria, India na Marekani.

Meneja Uhifadhi Taarifa na Machapisho Costech, Dk Philbert Luhunga anasema kwa kuwa lengo la serikali kupitia tume hiyo ni kuratibu sayansi, teknolojia na ubunifu pamoja na kutoa ufadhili wa fedha imeona ni jambo jema kutembelea miradi inayoifadhili ili kuielezea jamii matokeo chanya ambayo yameonekana kwa lengo ya kuzifahamu teknolojia na bunifu hizo iweze kuzitumia.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button