SMARTDARASA kidedea mradi wa Best Design Thinking Project
NAIROBI, KENYA: SMARTDARASA imepata nafasi ya kwanza katika mradi bora wa Best Design Thinking Project kwenye fainali za Mpango wa Youth African Leadership.
Smartdarasa ni mfumo wa kujifunza masomo ya Sayansi,Teknolojia,Uhandisi na Hisabati (STEM)kupitia uzoefu wa vitendo katika maabara ya kidigitali.
Mfumo huo hutumia teknolojia ya kisasa ya Medianuwai kama vile 2D, 3D, AI, AR, na VR, na kuwezesha wanafunzi na walimu kufanya majaribio na kukusanya data ndani ya mazingira ya maabara ya kidijitali, inayofanana na uzoefu wa maabara halisi.
Programu ya YALI ya wiki 4 iliwakutanisha washiriki 84 kutoka nchi 14 za Afrika, ikilenga mada muhimu kama vile Ufiki wa Ubunifu wa Kubuni, Uongozi wa Afrika, na mbinu bora za uwasilisho ambapo programu hiyo inafadhiliwa na USAID na inaendeshwa na Chuo Kikuu cha Kenyatta nchini Kenya.
Kampuni hiyo inajivunia kuwa kampuni pekee ya Tanzania iliyoteuliwa kuwania Tuzo za EdTechX za mwaka 2024 katika kipengele cha Mashariki ya Kati na Afrika ambapo washindi watatangazwa kwenye chakula cha jioni cha Tuzo za EdTechX mnamo Juni 18, 2024, katika Klabu ya Hurlingham jijini London.
Uteuzi huo unasisitiza athari kubwa na uwezo wa Smartdarasa katika sekta ya teknolojia ya elimu.