MAHAKAMA ya Wilaya ya Mlele mkoani Katavi imemhukumu mkazi wa Kijiji cha Kamguluki mkoani Mara kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kukiri kufanya kosa la kujifanya ndiye Diwani Athuman, Mkurugenzi wa Upelelezi na Usalama wa Taifa.
Hakimu Mkazi, Bilal Ahmed alimhukumu Raymond Bwire (28) baada ya kumtia hatiani kwa kosa hilo.
Ahmed alisema anatoa hukumu hiyo ili iwe fundisho si tu kwa Bwire lakini pia kwa wengine wanaofikiria kutenda kosa kama hilo linalochafua sifa ya maofisa wa vyombo vya dola.
Bwire alijifanya ofisa wa serikali kupitia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (SMS) akitaka kumtapeli Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlele, Theresa Irafy amwajiri mwanawe wa kiume ili awe mtumishi wa umma. Hiyo ilikuwa Agosti 10 mwaka huu.
Ilidaiwa pia mahakamani kuwa hata mtu ambaye Bwire alitaka aajiriwe si mwanawe.
Ilifahamika kuwa Irafy alivifahamisha vyombo vya dola vikamfuatilia Bwire na kumkamata mkoani Mara, kisha akapelekwa wilayani Mlele mkoani Katavi kujibu mashtaka.