SMZ kubadili mwelekeo wa utalii

Eneo la Mji Mkongwe, Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema imejipanga kubadili mwelekeo wa utalii kutoka katika maeneo ya fukwe na kwenda katika mabadiliko ya majengo ya kale ya historia ikiwemo miji ya urithi wa kale.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Simai Mohamed Said alisema hayo wakati akitoa mwelekeo wa wizara katika kukuza sekta ya utalii na kuitangaza Zanzibar kimataifa.

Said alisema utalii wa kutegemea msimu sasa umepitwa na wakati na Zanzibar inatakiwa kutumia utajiri wa vivutio vya utalii kuvutia wageni katika kipindi chote cha mwaka.

Advertisement

Alisema bado utalii wa magofu ya kale yaliyobeba historia za watawala haujatangazwa vizuri sanjari na majengo hayo kuwekezwa kumbukumbu.

Aliyataja magofu hayo kuwa ni pamoja na gofu la Mwinyimkuu lililopo Dunga Wilaya ya Kati ambalo limebeba historia ya mtawala wa kwanza wa kienyeji hata kabla ya kuja kwa Wareno na Waarabu.

Aidha, alitaja gofu lingine kuwa ni la Kwa Bi Hole lililopo Bungi, Wilaya ya Kati na Mkamandume lililopo Pemba na kwamba magofu hayo yanaonesha historia ya mambo ya kale ambayo watafiti wanaweza kuyatumia pia kufanya kazi zao.

”Zanzibar tumejaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii ikiwemo magofu ya kale yaliyobeba utajiri wa historia ya watawala mbalimbali waliopata nafasi ya kuongoza Zanzibar, lakini bado hatujaitumia vizuri,” alisema Said.

Aidha, aliiagiza Kamisheni ya Utalii Zanzibar ifungue milango zaidi na ihudhurie maonesho ya kimataifa ili kuinadi Zanzibar kimataifa.

Alisema maonesho ya kimataifa ni fursa nyingine muhimu sana za kuinadi Zanzibar katika ramani ya utalii duniani kwani kwa kawaida maonesho hujumuisha mawakala na wafanyabiashara wakubwa katika sekta ya utalii.

Kwa mfano aliyataja maonesho ya Berlin, Ujerumani na ya Uarabuni kuwa ni fursa ya kutangaza vivutio vya Zanzibar ili kushawishi mawakala wa utalii walete wageni.

”Nafasi ya kuitangaza sekta ya utalii kupitia utalii wa majengo ya kale ni kubwa ambapo kwa sasa tunatarajia kuanza ujenzi wa jengo la Beit-al-Jaib hivi karibuni ambapo wenzetu Oman wapo tayari,” alisema Said.

Katibu Mkuu Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, Fatma Mbarouk alisema filamu ya Royal Tour imeongeza idadi ya watalii na mashirika ya ndege ya kimataifa yameanza safari zake nchini.

”Matunda ya filamu ya Royal Tour yameanza kuonekana ambapo tayari yapo zaidi ya mashirika ya ndege 15 yameahidi kuanzisha safari zao za kimataifa,” alisema Mbarouk na kuongeza kwamba sekta ya utalii inaongoza kwa kuchangia pato la taifa ikiwa na asilimia 29 zisizofikiwa na sekta nyingine.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *