WIZARA ya Maji, Nishati na Madini imesema itahakikisha miradi inayotumia fedha za Covid-19 inakamilika kwa wakati ili kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.
Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi, Abdallah Hussein Kombo wakati akizungumza na watendaji wa wizara hiyo baada ya kutembelea miradi inayotekelezwa na wizara hiyo ikiwemo ya fedha za Covid-19.
Alisema serikali imetenga Sh bilioni 34.2 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji safi na salama ambayo lengo lake kumaliza tatizo la maji linalowakabili wananchi wengi.
Alisema kiwango cha upatikanaji maji safi na salama kwa upande wa Zanzibar kipo chini kwa asilimia 45 wakati kipaumbele cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya nane ni upatikanaji wa huduma hiyo ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2020-2025.
Aliitaka wizara hiyo kuhakikisha inakamilisha miradi inayotokana na ujenzi wa visima 38 vya usambazaji maji safi na salama ambayo imechukua muda mrefu sasa kukamilika kwake.
Aidha, aliitaka wizara kuhakikisha inalinda vyanzo vya maji safi na salama kwa kujenga uzio kuhakikisha vyanzo hivyo haviharibiwi na kuvamiwa na watu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za kudumu.
Akizungumza katika ziara hiyo, Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Shaibu Kaduwara alisema wamejipanga kikamilifu kutekeleza miradi inayotokana na utekelezaji wa ilani ya CCM pamoja na Dira ya Maendeleo 2030 ambayo imeweka kipaumbele katika upatikanaji wa maji safi na salama.
Alisema mipango ya wizara ni kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inapatikana kwa wananchi wote katika kipindi cha miezi sita ikiwemo kusimamia vizuri mradi wa maji unaotekelezwa na Benki ya Exim kutoka India.
”Wizara ya Maji tumejipanga katika kipindi cha miezi sita kuhakikisha tunapata huduma ya maji safi na salama kwa kutekeleza miradi ya uzalishaji maji ikiwemo matangi ya maji na uchimbaji wa visima,” alisema.
Mapema Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Salama (ZAWA), Salha Mohamed Kassim alizitaja miongoni mwa changamoto kubwa zinazoathiri maendeleo ya upatikanaji wa huduma ya maji safi ni uvamizi wa vyanzo na uharibifu wa miundombinu yake.
Wizara ya Nishati na Madini imetengewa Sh bilioni 34.2 ikiwa ni fedha za Covid-19 kwa ajili ya sekta ya maji safi na salama, ambapo kati ya fedha hizo Sh 6,781,660,000 ni kwa ajili ya ununuzi wa mashine za maji zipatazo 123.
Aidha, Sh 12,660,000,000 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa matangi ya kuhifadhi maji 10 katika vijiji vya Unguja na Pemba ikiwemo Uroa, Bumbwini pamoja na kisiwa cha Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja.