SMZ kujenga nyumba 72 za makazi

SHIRIKA la Nyumba la Zanzibar (ZHC) limetiliana saini na Kampuni ya Simba Development ya Dar es Salaam kujenga nyumba za makazi eneo la Mombasa kwa Mchina, Unguja ikiwa ni hatua ya kuwapatia wananchi makazi bora yenye nafuu.

Mkurugenzi Mkuu wa ZHC, Mwanaisha Ali Said akizungumza baada ya utiaji saini wa kuanza kwa mradi huo, alisema mradi huo unatarajiwa kuchukua takribani miezi 15 hadi kumalizika kwake ambapo nyumba 72 zitajengwa.

Alisema mradi huo unatarajiwa kugharimu Sh bilioni 9.8 ambapo shirika la nyumba litatoa Sh bilioni tatu na fedha nyingine zitatolewa kutoka mfuko mkuu wa serikali.

Alisema baada ya kumalizika kwa ujenzi wa nyumba hizo zitauzwa kwa wananchi watakaozihitaji kwa bei tofauti. Baadhi ya nyumba zitakuwa na vyumba vitatu na nyingine viwili.

”Huu ni mradi wa kwanza wa ujenzi wa nyumba za makazi unaotarajiwa kutekelezwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Hussein Mwinyi ambapo baadhi ya fedha zimetolewa na shirika na zipo ambazo zimetolewa na serikali kuu,” alisema.

Meneja wa Kampuni ya Simba Development, Nurdin Hussein alisema amefurahishwa na uamuzi wa shirika hilo kwa kitendo cha kuwaamini hatua ambayo imewapatia kazi ya kutekeleza mradi huo.

Aliahidi kutekeleza kazi hiyo kwa kuzingatia uwezo na ubunifu katika usanifu wa majengo ya makazi ya wananchi na kukidhi mahitaji ya makazi bora.

”Nachukua nafasi hii kulipongeza Shirika la Nyumba kwa kitendo cha kuniamini na kunipa kazi ya kujenga nyumba za makazi ya wananchi na naahidi kutekeleza kazi hiyo kwa uwezo na ubunifu wa hali ya juu,” alisema.

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Rahma Kassim Ali alisema ujenzi wa nyumba za makazi ni mwendelezo wa ahadi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Awamu ya Nane inayotokana na utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2020-2025 ya kuwapatia wananchi makazi bora.

Alisema ujenzi wa nyumba za makazi utaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba kwa kadri ya hali ya uwezo wa shirika pamoja na serikali.

 

Habari Zifananazo

Back to top button