SMZ kushirikiana na SADC uboreshaji wa mawasiliano

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema Tanzania itashirikiana na nchi nyingine za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuboresha huduma za mawasiliano.

Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi SMZ, Dk Khalid Mohamed alisema serikali itathmini pendekezo la Chama cha Wadhibiti wa Mawasiliano Kusini mwa Afrika (CRASA) kuhusu kupunguza gharama za mawasiliano kwenye ukanda wa SADC.

Mohamed alisema hayo jana wakati wa ufunguzi wa mkutano wa pili wa Kamati ya Udhibiti wa Uchumi (ERC) wa CRASA ulioratibiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Advertisement

“Kuhusu suala la roaming (kuunganisha mawasiliano ya simu kwa watumiaji walioko nchi tofauti) kama ulivyolizungumzia Mwakilishi wa Katibu Mtendaji wa CRASA, sisi pamoja na wenzetu tutaangalia namna ambavyo tutaweza kulitekeleza suala hilo ili kuwezesha wananchi wetu kupata gharama nafuu za Mawasiliano wanapokuwa kwenye nchi wanachama wa SADC,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari alisema wajumbe wa CRASA watapata fursa ya kuelewa masuala muhimu katika ukuzaji sekta ya mawasiliano, na TCRA itapata uelewa wa masuala yatakayosaidia usimamizi wa gharama za mawasiliano.

Kaimu Katibu Mtendaji Mkuu wa CRASA, Shukya Kiroga alisema utafiti wa kitaalamu wa gharama elekezi tayari umekamilika na kinachotakiwa ni nchi wanachama kuanza utekelezaji.

“Sisi kwa upande wetu tumetekeleza wajibu wetu kinachosubiriwa ni nchi wanachama waridhie kisha Utekelezaji wake uanze, hii nikiamini itapunguza pakubwa gharama za Mawasiliano kwenye ukanda wa SADC,” alisema Kiroga.

CRASA imekutanisha mamlaka 13 za usimamizi wa mawasiliano kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo ni Tanzania (TCRA), Zambia (Mamlaka ya Habari na Teknolojia ya Mawasiliano (ZICTA).

Nyingine ni Zimbabwe (Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Posta (POTRAZ), Afrika Kusini (Mamlaka Huru ya Mawasiliano (ICASA).

Pia Msumbiji (Taasisi ya Taifa ya Mawasiliano (INCM), Namibia (Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Namibia (CRAN), Eswatini (Kamisheni ya Mawasiliano (ESCCOM) na Malawi (Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Malawi (MACRA).