SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imewataka wananchi kuotesha miti ya aina mbalimbali ikiwamo mikoko pembezoni mwa bahari kukabili mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri maeneo wanayoishi watu na wengine kulazimika kuhama.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Harusi Said Suleiman wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Kojani, Hassan Hamad Omar kwa tiketi ya ACT-Wazalendo aliyetaka kujua serikali imejipanga vipi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Said alisema changamoto za mabadiliko ya tabianchi zimejitokeza kwa kasi katika maeneo mbalimbali na kutaja visiwa vidogo ambavyo baadhi ya wakazi wake wameanza kuhama.
Alisema mawimbi ya bahari yanayovuma pembezoni mwa fukwe yamesababisha athari kubwa huku shughuli za kilimo zikiathirika kutokana na maji ya bahari kuingia katika mashamba ya mpunga.
”Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inazifahamu vizuri athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo maji ya bahari kuvamia maeneo ya makazi ambapo tumeshuhudia mashamba ya kilimo yakiingiliwa na maji na wakulima kusitisha shughuli zao,” alisema.
Alitaja mikakati inayotarajiwa kuchukuliwa kwa sasa ni pamoja na kusambaza miche mingi ya miti aina ya mikoko yenye uwezo mkubwa wa kuzuia kasi ya maji baharini.
Alisema serikali imeanza kujenga madaraja na kuta za kuzuia maji ya bahari. “Tunawashajihisha wananchi kuotesha miti aina ya mikoko ambayo ni maarufu katika maeneo ya fukwe katika kuzuia kasi ya maji ya bahari kuvamia maeneo ya makazi ya wananchi,” alisema.
Zaidi ya maeneo 150 katika visiwa vya Unguja na Pemba yanakabiliwa na tishio la athari za mabadiliko ya tabianchi.
Baadhi ya visiwa vidogo ambavyo vipo katika tishio na kukabiliwa na mabadiliko ya tabianchi kiasi ya kutoweka ni pamoja na Mnemba kwa Unguja na Kisiwa Panza, Mtambwe mkuu kwa upande wa Pemba.