SMZ yapiga marufuku usafirishaji vyakula nje ya Zanzibar

Zanzibar

WAKATI Waislamu wakijiandaa na mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaotarajiwa kuanza wiki ijayo, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda imedhibiti mfumuko wa bei za vyakula na kupiga marufuku usafirishaji wa bidhaa za vyakula ikiwemo mchele kwenda Tanzania Bara hatua itakayotoa unafuu wa maisha.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Omar Said Shaaban wakati akitoa ufafanuzi kuhusu kupanda kwa bei za bidhaa na tatizo la mfumuko wa bei na njia za kukabiliana na tatizo hilo.

Alisema kumejitokeza wimbi la wafanyabiashara kutoka Zanzibar kusafirisha mchele unaoingia nchini kwenda mikoa jirani ya Tanzania Bara ikiwemo Tanga.

Advertisement

Shaaban alisema tatizo hilo lilisababisha ndani ya nchi kujitokeza kwa mfumuko wa bidhaa mbalimbali ikiwemo mchele pamoja na uhaba wake na kusababisha kupanda kwa bei hadi kilo moja kufika Sh 5,000.

Alisema hali ya chakula kwa sasa imerudi kama ilivyokuwa zamani  ikiwemo upatikanaji wa bidhaa hizo kwa wingi kama mchele, unga wa ngano pamoja na sukari kwa bei inayoridhisha.

Aliongeza kuwa hadi sasa bei ya mchele wa kawaida maarufu ”Mapembe” upo kati ya Sh 2,000 kutoka Sh 5,000 hadi 4,000 hali inayoridhisha kwa kiwango kikubwa,” alisema.

Mapema, Shaaban aliitaja mikakati mingine ikiwemo Tume ya kumlinda mlaji kuwatafuta wafanyabiashara wanaopandisha bei ya bidhaa katika maduka ya Unguja na Pemba.

Alisema hakuna sababu ya wafanyabiashara kupandisha bei ya bidhaa muhimu za chakula zaidi katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani unaotarajiwa kuanza katika wiki ijayo kwa sababu vyakula vipo vya kutosha.

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *