SMZ yataja vipaumbele 5 uchumi wa buluu

Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar,

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema ina vipaumbele vitano katika sera ya uchumi wa buluu ili kuimarisha uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Dk Aboud Jumbe alitaja vipaumbele hivyo kuwa ni utalii, uvuvi, usafiri wa baharini, nishati na usimamizi wa bahari.

Dk Jumbe alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) katika ofisi za makao makuu ya kampuni hiyo, Tazara, Dar es Salaam.

Advertisement

Alisema utalii umekuwa si kwa Zanzibar pekee bali kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini kwa Zanzibar utalii wa pwani umekuwa ukiongeza mapato ya nchi.

Dk Jumbe alitaja eneo lingine kuwa ni uvuvi na mazao ya baharini kwa maelezo kuwa asilimia kubwa ya wananchi wa Zanzibar wanaguswa na uchumi wa buluu ndani ya mikono yao katika sekta mbili muhimu ikiwemo uvuvi mdogomdogo na mazao ya baharini.

Alisema kitendo cha kuhakikisha kwamba wavuvi wadogo wanafaida na wanakuwa chachu ya msingi wa uchumi wa buluu kumeleta hamasa ya aina yake kwani serikali imeingia katika kiini hasa cha kuuondoa umaskini miongoni mwa wananchi wake.

Kipaumbele kingine alichokitaja ni usafiri wa baharini ambapo kuna bandari, miundombinu ya usafiri wa baharini, vyombo vya usafiri wa baharini, mchango wa kibiashara, mchango wa huduma wa usafiri wa baharini lakini pia usalama wa baharini.

“Nishati kwa Zanzibar kuna nishati na uchimbaji wa mafuta na gesi. Sera ya uchumi wa buluu imelenga katika jitihada za serikali za kuleta mageuzi katika uchimbaji wa mafuta na gesi kwa sababu ulimwenguni kote asilimia 30 ya uchimbaji wa mafuta na gesi hivi sasa unafanyika baharini. “Huko ardhini gesi inaanza kuisha, mafuta yanaanza kuisha sasa wanaingia kwenye buluu bahari, sasa buluu bahari imechukua asilimia 72 ya sayari nzima. Kule ndio kwenye maeneo ambayo bado hayajachimbwa kwa hiyo watu ndio wanasogea kule ndio maana ukiangalia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utakuta ni bahari,” alisema.

Kwa maelezo yake hicho ni kipaumbele si tu kinaipeleka Zanzibar mbele lakini pia Tanzania katika suala zima la utafiti, utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi katika bahari. Akimnukuu Rais Samia Suluhu Hassan Februari mwaka huu akiwa nchini Ufaransa, alitaka mataifa kukaa pamoja kuangalia suala zima la usimamizi wa bahari.

“Ni sehemu kubwa sana, huko kunaingia hifadhi ya bionowai, huko kunaingia mabadiliko ya tabianchi, usalama wa bahari magendo ya watu, magendo dawa za kulevya pamoja na masuala ya ulinzi lakini pia masuala ya uchumi wa buluu, nishati, utalii, usafiri wa baharini, hifadhi ya bahari masuala mengine yote sasa ni lazima nchi iwe na sera yake ya sera nzima ya uchumi wa bahari sio uchumi wa buluu pekee,” alisema.

Alisema kwa Zanzibar wameamua kuwa na mpango mkakati wa kitaifa kwa kuanza na wananchi wao katika kuwasaidia suala zima la uelewa, mbinu, zana, mitaji na masoko katika maeneo yao ya uvuvi mdogomdogo, ufugaji wa kaa, ufugaji wa kamba, ufugaji wa pweza kwa kuwa mambo yanayojenga jamii yanatengeneza mfumo mzuri wa mustakabali wa taifa.