Soka la Ufukweni wang’ara, watolewa

TIMU ya Taifa ya Soka la Ufukweni imemaliza mchezo wa hatua ya makundi kwa ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Mauritius katika mchezo wa mwisho hatua hiyo, michuano ya Baraza la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (Cosafa) uliochezwa jana nchini Afrika Kusini.

Matokeo hayo yameifanya Tanzania kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye Kundi B na Mauritius wakishika nafasi ya nne baada ya kupoteza michezo yote mitatu.

Licha ya kushinda bado hawana nafasi ya kusonga mbele baada ya kushindwa kufanya vizuri katika michezo miwili ya awali katika hatua hiyo.

Walipoteza dhidi ya Uganda mabao 4-2 na dhidi ya Misri mabao 4-3 na kupoteza ndoto zao za kufika fainali kwa mara ya pili mfululizo baada ya mwaka uliopita kucheza fainali.

Nahodha wa kikosi hicho, Jaruph Rajab aliibuka mchezaji bora wa mechi hiyo kutokana na kiwango bora alichokionesha na kuisaidia timu kupata matokeo mazuri.

Waliosonga mbele hatua ya nusu fainali kwenye Kundi B ni Misri na Uganda ambao wameshinda kila mmoja michezo miwili kabla ya jana kukutana wenyewe kwa mchezo wa mwisho wa kukamilisha ratiba.

Michezo ya nusu fainali inatarajiwa kuchezwa Septemba 30, mwaka huu na fainali itachezwa Oktoba mosi.

Habari Zifananazo

Back to top button