Soka yasambaza ujumbe unyonyeshaji na lishe Iringa

TIMU ya soka ya Makongoni FC ya mjini Iringa imenyakua kombe la mashindano ya wiki ya unyonyeshaji katika ngazi ya Mkoa wa Iringa baada ya kuibwaga Mshindo FC nayo ya mjini Iringa kwa mikwaju ya penati 4-2.

Fainali ya kombe hilo iliyoshuhudia timu hizo zikitoka sare ya bao 2-2 katika dakika tisini za mchezo huo kabla ya kupigwa kwa matuta hayo ilifanyika katika uwanja wa shule ya Msingi Mlandege mjini Iringa na kuhudhuriwa na kinababa wengi.

Ligi hiyo ya wiki ya unyonyeshaji iliyochezwa kati ya Agosti 1-7 ilishirikisha timu nane na kutumiwa na mkoa wa Iringa na wadau wake wa lishe kufikisha ujumbe wa unyonyeshaji katika kukabiliana na udumavu wa watoto kwa kina baba ambao ni mashabiki wa mchezo huo.

Wakati ripoti ya utafiti wa Hali ya Uzazi ya Afya ya Mama na Mtoto na Maralia ya mwaka 2022 ikionesha hali ya udumavu nchini imepungua hadi asilimia 30, mkoa wa Iringa umeendelea kujikongoja na tatizo hilo huku takwimu zikionesha unaongoza kitaifa kwa kuwa na asilimia 59.9.

Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu Februari 7, 2023 jijini Dodoma wakati akizindua ripoti ya awali ya viashiria vya afya ya uzazi na mtoto na malaria ya mwaka 2022 inaonesha mkoa wa Iringa unafuatiwa na mkoa wa Njombe wenye asilimia 50.4 na Rukwa wenye asilimia 49.8.

Afisa Lishe wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Stella Kimambo alisema ligi ya mpira wa miguu iliyozikutanisha timu mbalimbali za mjini Iringa imewawezesha kufikisha ujumbe kwa kinababa kuhusu umuhimu wao katika kuhakikisha mama anayenyonyesha anapata lishe bora na muda wa kupumzika.

“Mama anayenyonyesha anatakiwa kupata lishe bora kwasababu mahitaji ya virutubishi kwa ajili ya afya yake na kutengeneza maziwa ya mtoto ni makubwa,” alisema mbele ya mamia ya akina baba waliohudhuria fainali hiyo.

Afisa Lishe kutoka Wizara ya Afya, Elieth Rumanyika alisema maziwa ya mama ni chanzo kamili na chenye uwiano cha lishe kwa watoto, na uwapa virutubishi vyote muhimu, kingamwili, vimeng’enya kwa ukuaji na ukuaji bora wa mtoto na hivyo kuzuia udumavu.

Afisa Kilimo Mkuu na Mratibu wa Lishe wa Wizara ya Kilimo, Margaret Natai alizungumzia tatizo la udumavu katika mikoa hiyo akisema; “Tatizo sio upatikanaji wa vyakula, vyakula vipo vingi na vya aina nyingi; shida iliyopo ni namna vyakula hivyo vinavyotumiwa hivyo elimu zaidi inahitajika.”

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Iring, Dk Chrisantus Ngogi alisema; “Mkoa wetu unaendelea kuchakata takwimu hizo zinaoonesha katika kila watoto 100 walio chini ya miaka mitano watoto 56 wamedumaa, tunafanya utafiti wa kina zaidi kuangalia tatizo ni nini,” alisema.

Pamoja na mkoa wa Iringa kuongoza kwa udumavu, Dk Ngogi alisema mkoa wake umepiga hatua ya unyonyeshaji ukiwa na asilimia 66 ya unyonyeshaji wa maziwa pekee ya mama tofauti na takwimu ya jumla ya kitaifa ya asilimia 64.

Habari Zifananazo

6 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button