‘Soko Tanzania lisiwe la bidhaa duni’
DAR ES SALAAM; WAFANYABIASHARA nchini wametakiwa wasitumie soko la Tanzania kuingiza bidhaa zenye viwango duni, badala yake wasimamie ubora na viwango.
Katibu Tawala wa mkoa wa Dar es Salaam, Dk Toba Nguvila amesema hayo leo Dar es Salaam, huku akiliagiza Baraza la Ushindani (FCT) kutoa maamuzi kwa haki kupunguza migogoro na migongano.
Amesema Tanzania sio wa kutumia bidhaa zenye ubora hafifu na ndio maana lila bidhaa inayoingia serikali imeweka viwango vya ubora unaotakiwa na kinyume na hivyo ipo hatari ya mlaji kupata changamoto.
“Kwa mfano ninyi wafanyabiashara mnapoagiza mzigo maeneo mbalimbali, simamieni bidhaa zenye ubora, ili mlaji naye aweze kunufaika,” amesema.
Amesema jukumu la FCT pia kuhakikisha bidhaa zenye ubora na viwango zinazotakiwa na mlaji na kutakiwa kuongeza elimu kwa umma.
Kuhusu FCT amesema inawajibu wa kutoa suluhu ya maamuzi mbalimbali yanayolalamikiwa na walaji na kuwataka wafanyabiashara kutumia taasisi hiyo ili kupata haki zao.
Kwa upande wake Msajili wa Baraza, Renatus Rutta amesema FCT Ina muundo wa kimahakama na inashughulikia rufaa kutoka taasisi mbalimbali na kutoa maamuzi.
Amesema baraza hilo lipo kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanapata haki zao zinazostahili na kamwe wasifikie hatua ya kukwama kwa kuwa maamuzi yao ni ya mwisho.
Amesema tangu kuanzishwa baraza hilo tayari limepitia mashauri 442 na kati ya hayo mashauri 429 yametolewa uamuzi ambayo ni sawa na asilimia 97.
Baraza hilo lina jukumu la kupokea, kusikiliza na kuamua kwa haraka rufaa zitokanazo na mashauri ya ushindani yatokanayo na maamuzi yanayofanywa na Tume ya Ushindani (FC)C na Mamlaka za udhibiti ambazo ni EWURA, TCAA, TCRA, LATRA NA PURA.