Soko la Vetenari karibu kutumika

WAFANYABIASHARA wa Soko la Vetenari mkoani Dar es Salaam wataanza kutumia soko hilo ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa.

Hayo yalielezwa Alhamis na Mwenyekiti wa soko hilo, Daniel Mlangu alipozungumza na HabariLEO lililotaka kujua hatua ya ujenzi wa soko hilo lililoungua moto Mei 30, 2022 na kuteketeza bidhaa zote na miundombinu ya soko hilo zimefikia wapi.

“Hadi sasa ujenzi umekamilika kwa asilimia 98 kutokana na juhudi ambazo zimefanywa na serikali, huu ni upendeleo wa kipekee ambao tumepatiwa katika soko hili, ila kuna vitu vichache havijakamilika kama umeme na kuweka nilu lakini tunatarajia vitakamilika hivi karibuni,” alisema.

Vetenari ni soko linalotoa huduma ya kuuza chuma chakavu na matunda mbalimbali kwa jumla yakiwemo matikitimaji, maembe, mananasi na kusafirishwa katika nchi mbalimbali kama vile Malawi, Uganda, Kenya, Msumbiji na wafanyabiashara mbalimbali mkoani Dar es Salaam.

Mlangu alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwatengea fedha kupitia asilimia kumi za halmashauri ambazo kwa namna moja zimefanikisha ujenzi wa soko hilo ndani ya muda mfupi kuliko ilivyotarajiwa.

Mmoja kati ya wafanyabiashara kutoka katika soko hilo, Juma Seleman ameipongeza serikali kwa ujumla kwa kutambua uwepo wa wananchi kwa kutatua kero na matatizo mbalimbali ambayo yanatokea kwa jamii.

Ujenzi wa soko hilo umegharimu Sh milioni 207 ambazo zimetolewa na serikali kwa ajili ya kuhakikisha wafanyabiashara wanaendelea na shughuli zao za kibiashara kama ilivyokuwa ada mara baada ya kukamilika kwa ujenzi huo.

 

Habari Zifananazo

Back to top button