SOKOINE: Urithi wa taifa katika uongozi, uadilifu

“HAYATI Edward Moringe Sokoine alikuwa mstari wa mbele na alisimama kidete kukemea rushwa akionesha wazi kuichukia.

“Alichukua hatua dhidi ya wala rushwa, walanguzi na wahujumu uchumi…. Aliwataka viongozi wa serikali na wananchi kueleza mali walizo nazo wamezipata namna gani na walipopata mali kwa njia haramu walimwogopa …” Ndivyo alivyosema Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko katika Mdahalo wa Kitaifa wa Kumbukizi ya Miaka 40 ya Edward Moringe Sokoine uliofanyika Aprili 8, 2024 katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Kampasi ya Edward Moringe mjini Morogoro.

Kaulimbiu ya Kumbukizi ya Miaka 40 ya Sokoine: Urithi wa Taifa katika Uongozi Wake, Bidii, Uadilifu na Uaminifu”. Sokoine alifariki dunia kwa ajali ya gari Aprili 12, 1984.

Katika mdahalo huo alipokuwa mgeni rasmi, Dk Biteko ambaye pia Waziri wa Nishati, alizungumzia namna wahujumu uchumi walivyoujua na kuuogopa uongozi imara wa Sokoine akiwa Waziri Mkuu akisema:

“Watu walitupa fedha na mali nyingine za thamani kuogopa kukamatwa na kuhojiwa… Sokoine hakuwa adui wa ubepari, alikuwa rafiki wa ubepari wa kweli na alikuwa adui wa ubepari wa uongo”.

Katika kumbukizi hiyo, Biteko anasema Sokoine atakumbukwa kwa kuwa kinara wa mapambano dhidi ya rushwa na uhujumu uchumi pamoja na uzalendo wake katika kuipigania Tanzania kwa moyo wake wote.

Profesa mstaafu wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Issa Shivji katika mada yake anarejea hotuba aliyoitoa Sokoine katika Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1982 akitaja mambo matatu aliyoyasisitiza Sokoine.

Shivji anayataja mambo hayo kuwa ni umuhimu wa kujitosheleza kwa chakula, soko la ndani na kujitegemea. Anasema hizo ndizo alama kuu za maendeleo alizoacha Hayati Sokoine.

Hayati Edward Sokoine

Kwa mujibu wa Profesa Shivji, Sokoine alisisitiza mbele ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere akisema: “Huwezi ukawa nchi huru kama hujitegemei kwa chakula, kama huwezi kujiamulia mambo yako mwenyewe, bila shaka utakuwa unatekeleza maagizo ya yule unayemtegemea kwa lishe yako. Hii ndio maana ya kulinda uhuru wako.”

Ndio maana Shivji anashauri kuangaliwa kwa sera za nchi zinazohusu uwekezaji, ujenzi wa maghala ya kuhifadhi chakula, upangaji wa bei ya vyakula, ununuzi, usafirishaji wa chakula kutoka eneo moja kwenda lingine akitaka zilenge katika kujitosheleza kwa chakula.

Anataja jambo lingine kuwa ni dhana ya kujitegemea akisema: “Sokoine hakumaanisha kujitegemea kwa kaya pekee, bali kujitegemea kama Taifa….”

Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba anasema wakati Sokoine anateuliwa kuwa waziri mkuu kwa kipindi cha kwanza, yeye alikuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na alifanya naye kazi kwa karibu.

Kwa mujibu wa Warioba, Sokoine aliandaliwa kuwa mwaminifu kwa nchi yake, mwenye nidhamu na mchapa kazi.
Kwamba, Sokoine alikuwa kiongozi mfuatiliaji aliyeamini kuwa, kiongozi kwa imani yake, lazima awe na uwezo wa kufanya kazi anayopewa na anapooona hana uwezo nayo, aseme ukweli na asikubali kuipokea.

“Sokoine alionesha kwa mfano pale alipokataa kuzitumikia baadhi ya nyadhifa alizopewa. Sijui ni wangapi wanaweza kupata nafasi wakakataa kwa kuwa wanajua hawawezi kuitumikia ipasavyo,” anasema Warioba na kuongeza kuwa, Sokoine aliamini kiongozi anapaswa kujiamini kwamba atafanya sawia kazi aliyopewa.

Kuhusu uadilifu, Warioba anamtaja Hayati Sokoine kama kiongozi ambaye enzi za uhai wake alikuwa anafuatilia maagizo ya viongozi wake na yale anayotoa kwa watendaji.

Warioba anasema, Sokoine alitaka wakulima wapate zana mapena kama mapanga, majembe na mbolea. Alitaka uagizaji wa zana hizo kutoka nje ya nchi ufanyike mapema ili zimfikie mkulima kwa wakati.

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, Sokoine ndiye alianza kuwapa elimu wafugaji wa Kabila la Wamasai kuhusu umuhimu wa kuacha kutumikia mifugo, badala yake mifugo ndiyo iwatumikie wao ili wanufaike kiuchumi.

Makamu Mkuu wa SUA, Profesa Raphael Chibunda anasema awali chuo hicho kingeitwa Chuo Kikuu cha Morogoro cha Kilimo, lakini ili kumuenzi Sokoine, serikali ilibadili jina la chuo Julai 1, 1984 kwa Sheria ya Bunge Namba 6 ya Mwaka 1984 na kuwa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA).

Sokoine alisimamia kuanzishwa kwa chuo kikuu hicho mahususi kwa utoaji mafunzo na kufanya utafiti ili kutatua changamoto za kilimo nchini.

Anasema Sokoine alikuwa kiongozi wa kipekee hasa katika utoaji na usimamiaji wa uamuzi, uzalendo, uchapakazi, uadilifu na uaminifu aliyefanya kazi bila kuchoka kuhakikisha nchi inapiga hatua katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

“Moja ya sekta alizosimamia kwa nguvu zote ni sekta ya kilimo …sekta hii inaajiri Watanzania zaidi ya asilimia 65,” anasema Chibunda.

Anasema lengo kuu la mdahalo huo lilikuwa kukumbuka na kutoa taarifa kwa umma na kizazi kipya kuhusu mambo ambayo taifa letu limerithi kutoka kwa Sokoine yakiwemo ya uongozi bora, uzalendo, uadilifu uaminifu na uchapakazi.

“Uongozi bora ni moja ya nguzo muhimu katika maendeleo na tafiti zinaonesha uhusiano mkubwa kati ya uongozi bora na maendeleo ya nchi maana nchi zilizo na uongozi bora na imara zina maendeleo makubwa,” anasema Chibunda.

Anaongeza: “Serikali ya Awamu ya Kwanza iliyoongozwa na Mwalimu Nyerere iliamini kuwa moja ya nguzo muhimu katika maendeleo, ni uongozi bora”.

SOKOINE NI NANI

Edward Moringe Sokoine alikuwa waziri mkuu katika Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Mwalimu Julius Nyerere kwa vipindi viwili Februari 13, 1977 hadi Novemba 7, 1980 na alipoteuliwa tena Februari 24, 1983 na kutumikia Watanzania katika wadhifa huo hadi Aprili 12, 1984 alipofariki dunia kwa ajali ya gari eneo la Dakawa wilayani Mvomero (zamani Wilaya ya Morogoro) akitokea Dodoma kwenda Dar es Salaam baada ya kuahirisha kikao cha Bunge.

Alizaliwa Monduli mkoani Arusha na kupata elimu ya msingi na sekondari katika miji ya Monduli na Umbwe tangu mwaka 1948 hadi 1958.

Mwaka 1961 alijiunga na chama cha TANU (Tanganyika African National Union) baada ya masomo katika Uongozi nchini Ujerumani mwaka 1962 hadi 1963. Aliporejea nchini kutoka Ujerumani, alikuwa Ofisa Mtendaji wa Wilaya ya Masai, kisha akachaguliwa kuwa Mwakilishi wa Jimbo la Masai.

Mwaka 1967 alikuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Usafiri na Kazi na Mwaka 1972 alikuwa Waziri wa Usalama. Mwaka 1975 alichaguliwa kwenye Bunge wakati huo kupitia Jimbo la Monduli.

Miaka miwili baadaye akawa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hatimaye mwaka 1977 akawa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Habari Zifananazo

Back to top button