Spika aagiza itafutwe njia kusambaza mbolea ya ruzuku

SPIKA wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameiagiza Wizara ya Kilimo itafute njia au mawakala mbadala wasambaze mbolea baada ya serikali kufuta leseni za mawakala zaidi ya 736 waliotuhumiwa kuhusika na udanganyifu wa mbolea ya ruzuku.

Dk Tulia amesema hayo baada ya Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu (CCM) kuomba mwongozo kuliomba bunge lisimamishe shughuli lijadili kuhusu changamoto ya wakulima kukosa mbolea baada ya mawakala kati ya 736-800 kufutiwa leseni za usambazaji.

Dk Tulia alisema serikali imefanya uamuzi sahihi kufuta leseni za mawakala wadanganyifu kwenye mbolea ya ruzuku iliyotolewa na serikali.

“Wizara ya kilimo kwa maeneo mliyowafutia mawakala leseni za kusambaza mbolea mtafute wengine au njia mbadala ya kusambaza mbolea na iwafikie wananchi kwa wakati,” alisema.

Alisema serikali isiwarudishie leseni mawakala wadanganyifu kwa sababu wizi hawaruhusiwi.

“Kama kuna udanganyifu katika mbolea ya ruzuku ni haki ya serikali kuwafutia leseni, hata bunge limekuwa likipiga kelele na kupinga vitendo hivyo vya udanganyifu na kuibia serikali. Kwa serikali kuwafutia leseni mawakala hao ni jambo zuri, kama ambavyo sisi kama bunge tunavyopigia kelele,” alisema Dk Tulia.

Alisema zipo athari kutokana na idadi kubwa ya mawakala kufutiwa leseni hivyo lazima Wizara ya Kilimo itafute njia mbadala ili kuwasambazia wananchi mbolea.

Awali, Msambatavangu alisema kufutwa kwa leseni za mawakala kumesababisha wakulima wanaohitaji mbolea kwa ajili ya kupandia na kukuzia kukosa.

Mbunge huyo alisema alifahamu kwa nini wamefutiwa leseni baada ya kuzungumza na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ambaye alimweleza ni kutokana na kufanya udanganyifu katika mbolea ya ruzuku.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button