Spika aagiza uchambuzi hoja za CAG

SPIKA wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameziagiza kamati za kudumu za bunge zinazohusika na matumizi na fedha za umma zifanye uchambuzi kubaini ni kiasi gani hoja zilizowasilishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zimetekelezwa.

Kamati zinazoshughulikia matumizi na fedha za umma ni ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

Akiwasilisha taarifa bungeni Dodoma jana, Dk Tulia alisema kamati hizo zitapewa muda wa kufanya mapitio ya maazimio hayo na kuwasilisha taarifa bungeni ndani ya kipindi cha siku sita za kuhitimisha Bunge la Bajeti kwa mujibu wa Kanuni namba 124.

Aliwaeleza wabunge kuwa kama alivyolijulisha Bunge amepokea taarifa ya serikali kuhusu utekelezaji wa maagizo ya Bunge kuhusu utekelezaji wa maagizo yaliyotokana na ripoti ya CAG ya mwaka 2020/2021 kwa kuzingatia taarifa za kamati za PIC, PAC, LAAC zilizowasilishwa bungeni Novemba mwaka jana.

β€œIli Bunge lipate mrejesho mzuri, ninaelekeza kwamba kamati zinazohusika mara baada ya kumaliza uchambuzi wake, ziandae taarifa ambayo zitawasilishwa bungeni wakati wa kipindi cha siku sita za majumuisho ya bajeti kwa mujibu wa Kanuni ya 124,” alisema Dk Tulia.

Alisema utaratibu huo utaliwezesha Bunge kutekeleza jukumu la kuisimamia serikali kwa kuelewa ni namna gani imetekeleza maazimio yanayotolewa na Bunge kuhusu taarifa inayotolewa kila mwaka na CAG.

 

Habari Zifananazo

Back to top button