SPIKA wa Bunge, Dk Tulia Ackson amewashukia viongozi wanaonunua shahada za udaktari (PhD) wa heshima na kuwataka kujitafakari kwa hicho wanachokifanya, kwani hakina afya kwa mustakabali wa taifa.
Tulia ameyasema hayo bungeni mjini Dodoma baada ya Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi kuomba muongozo akiihoji vyuo vinavyotoa PhD hizo za heshima kama zinatambulika kisheria na mamlaka za elimu.
Akiitolea ufafanuzi suala hilo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Aldof Mkenda alisema kuna aina tatu za PhD, moja ni ya kusoma darasani na kufanya utafiti, ya pili ni ya kufanya utafiti chini ya uangalizi wa maprofesa wa vyuo husika vinavyotambulika na ya tatu ni ya heshima, ambayo anapewa mtu kutokana na mafanikio katika jambo fulani.
“Sasa hizi walizopewa wenzetu kama kuna uhitaji wa kufahamu vyuo walivyowapa kama vinatambulika au la tunaweza kufanya hivyo kupitia TCU, lakini kama mtu kapewa tu huko na hakuna uhitaji sisi hatuwezi zuia au kuverify kila mtu anayepewa, kukiwa na uhitaji Yes tutafanya hivyo bila shida, ” amesema Waziri Mkenda.
Akikazia suala hilo, SpikaTulia amesema ifike mahali wao kama viongozi wawe na haya, wajue jamii inawangalia kama kioo masuala ya kununua vyeti waachane nayo.
“Kama taifa ifike mahali tujue tunataka nini? Athari zake tunaweza tusizione sasa tukaziona kesho, UDSM inapompa Rais degree ya falsafa ya heshima ujue kuna proposal imeandikwa, jopo linakaa linafanya tafiti ya kazi alizofanya tangu alipoanza kufanya kazi mpaka alipofika, wanapima kwa vigezo vyao kama anafaa kupewa au la.
“Iitafika mahali wanaolipa pesa Dola 2500 hawatakua na tofauti na anayopewa Rais. Halafu mna watoto, mmewapeleka shule ili wasome waelimike tena mnawakazania kusoma kwa bidii, huku nyie mnanunua vyeti, mnapeleka watoto shule kufanya nini? mnawafundisha nini watoto wenu? Kwamba elimu haina maana watafute pesa wanunue cheti.
“Waheshimiwa Wabunge, vyuo vinavyotambulika havitoi degree kila wiki kila mwezi, uliza UDSM au UDOM toka wameanza wametoa degree za falsafa mara ngapi?
“Sio tu vyuo vya nje wanakuja na makabrasha yao ya vyeti wanaviuza kama pipi, kana kwamba vyuo vyetu havina umuhimu, kama taifa tuweke mwongozo mzuri, Tanzania sio kijiji vinakotoka hivyo vyeti wangeanza kutoa huko nchini kwao, wageni kuja na kuuza vyeti vyao kama pipi hapa ni kutuvunjia heshima kama nchi.
“Hata hivyo siwazuii kuendelea na utaratibu wenu wa kununua vyeti,” amesema Tulia.