Spika ataka ulinzi mazingira ya bahari

WIZARA ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu imetakiwa kuhakikisha inakamilisha mpango wa matumizi bora ya bahari na rasilimali zake kwa ajili ya kuepuka uharibifu wa mazingira baharini.

Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid alisema hayo Unguja wakati akifungua mafunzo kwa wajumbe wa baraza hilo kuhusu mpango wa matumizi bora ya bahari na rasilimali zake kwa ajili ya uchumi wa buluu.

Maulid alisema wakati Zanzibar ikitangaza sera ya kuelekea uchumi wa buluu, matumizi sahihi ya bahari yanahitajika kuwekewa mikakati madhubuti ili rasilimali zilizomo ziwe endelevu na kulindwa kwa faida ya vizazi vijavyo.

Advertisement

Alisema bado yapo matumizi mabaya yasiyozingatia rasilimali za bahari ikiwamo uvuvi haramu unaoharibu maisha ya viumbe vya baharini hususani matumbawe.

Aidha, alisema hadi sasa upo uvuvi uliopigwa marufuku ambao umeanza kutumiwa na wavuvi kitendo ambacho ni tishio kwa mazingira ya baharini na maisha ya viumbe .

”Tunahitaji kuja na mipango madhubuti ya kulinda mazingira ya baharini  zaidi wakati tukielekea katika kutekeleza sera ya uchumi wa buluu ambayo inahusisha mambo mengi kwa wakati mmoja”alisema.

Waziri wa Uvuvi na Uchumi wa Buluu, Suleiman Masoud Makame alisema sera ya uchumi wa buluu ipo katika hatua za mwisho kupelekwa kwa wadau. Alisema miongoni mwa mambo muhimu iliyozingatia ni mikakati ya kulinda rasilimali endelevu za baharini ikiwamo kupambana na uvuvi haramu ambao ni tishio kwa uhai wa samaki na matumbawe.

Alisema katika kuelekea uchumi wa buluu, uvuvi na uimarisha wa mazao ya baharini ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  ili kuhakikisha wananchi wanavuna hazina hiyo na kunufaika kiuchumi.

Makame  alisema kwa upande wa wakulima wa mwani ambao wamepewa kipaumbele, boti 500 zimekamilika huku 250  zikikabidhiwa kwa walengwa hatua itakayosaidia kuimarisha kilimo hicho ambacho asilimia 90 wanaokifanya ni wanawake.

“Jumla ya kampuni nane tumezipa kazi ya kutengeneza boti za uvuvi wa bahari kuu na nyingine za kilimo cha mwani ambapo matarajio yetu makubwa zitawanufaisha walengwa na kulima kilimo cha kisasa chenye tija,” alisema.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetenga Sh bilioni 34 kwa ajili ya kujikita na kuimarisha sekta ya uchumi wa buluu.