Spika ataka utaratibu ajira wanaojitolea kazini
SPIKA wa Bunge Dk. Tulia Ackson ameitaka serikali itafute utaratibu wa mpito wakati ikijipanga kwa ajili ya wafanyakazi wanaojitolea lakini hawapewi kipaumbele katika ajira.
Dk Tulia ametoa kauli hiyo bungeni leo, baada ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete kujibu swali la Mbunge wa Kiteto Edward Olele Kaita, aliyehoji lini serikali itapeleka bungeni marekebisho ya sherioa ya Ajira na Utumishi wa Umma kwa kigezo cha kujitolea ili kutoa fursa kwa wanaojitolea.
“Katika kipindi hiki cha kusubiri wakati serikali mkijipanga,maadam wapo hizo kada mbalimbali za watu wanaojitolea, kwenye hayo maeneo, mtafute utaratibu wa muda au wa mpito wa kuwatazama hao wakati mnasubiri kufanya hayo marekebisho makubwa, kwa sababu wako kule wanaendelea kujitolea” amesema Spika.
Akijibu swali la msingi la Mbunge huyo, Naibu Waziri Ridhiwani amesema kwa sasa serikali inafanya mapitio ya Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298, Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma, Toleo la Pili la Mwaka 2008, Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2022 na Miongozo inayohusu masuala mbalimbali ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma likiwemo suala la Ajira.
“Katika eneo la ajira, lengo la mapitio haya ni kuhakikisha serikali inaongozwa na utaalamu na weledi ”meritocracy” na usawa wa fursa za ajira kwa Watanzania wote.
Wakati serikali inaendelea na mchakato wa mapitio ya Sheria ya Utumishi wa Umaa itawashirikisha wadau wote muhimu kupata maoni yao.
Endapo itabainika bayana kigezo cha kujitolea kitatakiwa kuingizwa katika marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma, Serikali italeta muswada wa marekebisho wa sheria hiyo bungeni,” amesema Naibu Waziri.
Amesema kwa hatua ya sasa Serikali imeandaa mwongozo unaoweka mazingira wezeshi kwa vijana wanaohitimu katika vyuo mbalimbali kujitolea katika taasisi za umma kwa lengo la kuwawezesha kujipatia uzoefu utakaomwezesha katika ushindani pindi nafasi mbalimbali zinapotangazwa.
“Mwongozo huu utaziba ombwe lililokuwepo kutokana na kutokuwa na utaratibu mmoja ndani ya taasisi za umma kuhusu kujitolea,” amesema.