Spika atoa maelekezo hoja za suala la ushoga

Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson

SIKU moja baada ya wabunge kutaka wapelekewe wataalamu bungeni wa kuwapima masuala ya ushoga, Spika wa Bunge Dk TuliaAckson,  ametoa tamko la kuiagiza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuangalia  namna ya kufanya utafiti kupitia tume ya kurekebisha sheria.

Dk Tulia amesema wizara hizo zikae na kuona ni mambo gani yafanyiwe marekebisho, yaongezeke hivi sasa katika sheria ya makosa ya kujamiiana na sheria ya makosa ya jinai kusiwepo na mapungufu.

“Hatutataka kutunga sheria kwa mihemko, tunataka kutunga sheria tukiwa tunaelewa tatizo (la ushoga) ni kubwa kiasi gani katika jamii, kwa maana tunasema tatizo limeongezeka, lakini hatujui limeongezeka kwa kiasi gani, ” amesema Tulia na kuongeza:

Advertisement

“Yapo mambo ambayo kwa ufahamu wetu tunafahamu mambo hayo yanatokea sehemu nyingine, lakini hapa kwetu yapo na ni mabaya sana. Nafikiri kadri tunavyozungumza tusijikute ndio tunayakaribisha hayo mambo kwa kufungua ule wigo.

“Nafikiri tumekubaliana kwamba jambo hili (la ushoga) limeshasikika na kueleweka. Tumesikia viongozi wa dini, viongozi wa serikali na wananchi wakilizungumzia. Kwa muktadha huo serikali imeelewa kitu gani cha kufanya katika jambo hili,” amesema.

Kauli ya Tulia imekuja baada ya jana jioni Wabunge kutaka serikali ichukue hatua za haraka kuhusu suala hilo na huku wakipendekeza wabunge wote wapimwe ushoga na usagaji, kabla ya kuingia bungeni na iwe lazima kama ilivyokuwa chanjo ya Covid 19.

Wabunge hao Janeth Masaburi, Kunti Majala, Katani Ahmed na Joseph Kasheku ‘Musukuma’ walicharuka na kudai kuwa hata bungeni na baadhi ya viongozi wanajihusisha na matendo hayo.

Akirejea maandiko ya kwenye biblia katika kitabu cha mwanzo kuhusu kisa cha sodoma na gomora, Mbunge wa kuteuliwa Janeth Masaburi,  alidai kuwa wanaotetea ndoa na mahusiano ya jinsia moja ni  mke wa Lutu wa kwenye biblia ambaye aligeuka jiwe la chumvi.

“Kuna watu wengi ni wake wa Lutu humu, wanatetea ushoga, alipo shoga kuna basha, mashoga wanaonekana kwa urahisi, mabasha wapo wapi?  …mabasha hawawezi kutambulika na ndio wenye pesa…wahasiwe…kabla hawajahasiwa wachapwe viboko hadharani kama tulivyoona kwa Wahindi….Uganda na Wamasai waliomchapa yule mtu aliyewasaliti.

“Wengine ni viongozi tunawajua..waache.. tunamuongopa Mungu tu na si wanadamu…sisi wanadamu si kitu tupo duniani lakini kizazi lazima tukiendeleze,” amesema.

Naye Mbunge wa Kibamba Issa Jumanne Mtemvu akiomba taarifa  amesema: “kwenye eneo la maadili si tu wazazi nyumbani, si tu serikali kutengeneza mfumo,  inasemekana hata ndani ya bunge hili, sina uhakika inasemekana wapo.”

Kwa upande wa Mbunge wa Tandahimba, Katani Ahmed akichangia hoja alisema  wabunge ni kioo cha jamii na kumshauri Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kupeleka wataalamu bungeni ili wabunge wote waweze kupimwa.

“Mheshimiwa Mwenyekiti (Daniel Sillo) kukiwa na magonjwa ya mlipuko kama Covid, Ebola tunaona serikali inakimbilia kufunga mipaka na kuwekeza nguvu kubwa kukabiliana na mlipuko, hili suala la ushoga kwa sasa hivi ni janga.

“Wabunge ni kioo cha jamii kabla hatujatoka huko nje kupaza sauti kwa wananchi wetu tunatakiwa kuanza na sisi kwanza, Mhe Ummy (Waziri wa Afya), tuletee wataalamu humu wakae pale mlangoni hakuna kuingia bungeni mpaka uwe umepimwa, iwe kama kipindi cha Covid 19 kila mtu lazima achanjwe hakuna kusafiri mpaka uchanjwe na humu bungeni iwe hivyo.

Mbunge wa Viti Maalum Kunti Majala alisema: “Madaktari waletwe Jumatatu humu wabunge wote tupimwe, ili tuweze kutoka mbele ya jamii na kupaza sauti kukemea ushoga.

Kwa upande wa Musukuma alisema: “Hili bunge lipo ‘live’  tukizungumzia ufisadi watu wanasikiliza, tukizungumzia ushoga mnafanya masihara, mnataka lifanyike kimya, magonjwa ya mlipuko serikali inachukua hatua haraka kwa nini ili kuna ugumu?” Alihoji.

/* */