Spika Tulia atoa msaada wa Sh milioni 100

SPIKA wa Bunge ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson ametoa msaada wa Sh milioni 100 kwa wanawake 1,000 kutoka katika halmashauri saba za Mkoa wa Mbeya.

Hafla ya kukabidhi fedha hizo imefanyika Machi 4,2023 kwenye viwanja vya Ruanda Nzovwe jijini Mbeya na kuhudhuriwa na viongozi mbaimbali wa Chama Cha Mapinduzi na Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa aliyemuwakilisa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Zuberi Homera.

Uwezeshaji huo ni mwaka wa tatu mfululizo kwa Dk Tulia kutoa fedha kwa wanawake wajasiliamali ambapo mwaka wa kwanza aliwawezesha wanawake 400.

Kwa mwaka jana (2022) wanawake zaidi ya 600 waliwezeshwa na kwa mwaka huu (2023 ) wanawake 1,000 wamewezeshwa na kufanya jumla ya wanawake 2,000 kunufaika na misaada hiyo.

Dk Tulia amewaambia wananchi kuwa amedhamiria kubadilisha maisha yao kwa nguvu zake zote ili kutengeneza historia ambayo haijawahi kutokea katika mkoa huo ikiwemo kuyagusa maeneo mbalimbali.

“Mungu akituwezesha mwakani tutaongeza idadi na si hawa waliopata leo, tumekuwa tukizigusa kila sekta na tutaendelea kuhakikisha tunaboresha maisha ya kila mwananchi wa Mbeya” alisema Dk Tulia

Naye Mwenyekiti wa Bajaji ,Festo Mwasimba amemshukuru Dk Tulia kwa namna ambavyo siku zote anahangaika kuhakikisha anawakwamua kiuchumi wananchi wake bila kujali nafasi zao za kidini na kiitikadi ( chama ).

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodaboda Jiji la Mbeya , Aliko Fwanda amesema tangu Dk Tulia achaguliwe kuwa Mbunge, vijana wengi wamejiajiri na kumiliki pikipiki zao hivyo kama vijana hawatakubali kumpoteza kwa namna yoyoye ile.

Habari Zifananazo

Back to top button