Spika: Wabunge lipeni madeni TBA

SPIKA wa Bunge, Dk Tulia Ackson amewataka wabunge wote wanaodaiwa kodi na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kulipa mara moja kabla ya kutolewa kwenye nyumba za wakala huo.

Dk Tulia alitoa agizo hilo bungeni Dodoma jana katika kipindi cha maswali na majibu, baada ya Mbunge wa Viti Maalumu, Asha Abdullah Juma (CCM) katika swali lake la nyongeza kuitaka TBA kukarabati nyumba zake ambazo nyingi zimechakaa hususani za Dodoma.

“Nyumba za TBA hususani hapa Dodoma zimejengwa muda mrefu na nyingi zimechakaa, je, lini zitaboreshwa ili kuwa salama kwa watumiaji?” Alihoji.

Kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete ajibu swali hilo, Spika alieleza kuwa wakala huo unashindwa kufanya majukumu yake kutokana na madeni iliyonayo.

“Ninasema hivyo kwa kuwa wabunge nina barua zenu zinazoonesha mnadaiwa kodi na TBA. Wabunge wengi mnaodaiwa nawaagiza mkalipe msije mkafukuzwa huko ili TBA nayo itimize majukumu yake,” alisema.

Akijibu swali hilo, Mwakibete pia alibainisha kuwa wakala huo umekuwa ukidai watumishi wengi wa serikali jambo linalokwamisha shughuli zake nyingi ikiwemo kukarabati nyumba zake.

Awali, katika swali lake la msingi Mbunge wa Chaani Usonge, Hamad Juma (CCM) alitaka kujua serikali ina mpango gani kupitia TBA kuwajengea nyumba watumishi wa serikali wa Muungano kwa upande wa Zanzibar.

Mwakibete akijibu swali hilo, alisema moja ya jukumu la TBA ni kukarabati na kujenga nyumba na majengo ya serikali kwa ajili ya makazi kwa watumishi wa umma Tanzania Bara.

“Jukumu la ujenzi wa nyumba kwa watumishi wa umma kwa upande wa Zanzibar liko chini ya Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA),” alisisitiza.

Hata hivyo, alisema TBA na ZBA wanashirikiana na kushauriana kwenye mambo mbalimbali ya kitaalamu na kujengeana uwezo.

 

Habari Zifananazo

Back to top button