Spika: Waliotajwa na CAG hawatapona

 SPIKA wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema watuhumiwa wa ubadhirifu wa mali za umma waliotajwa katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ikithibitika ni kweli, watashughulikiwa ipasavyo.

Dk Tulia alisema hayo bungeni Dodoma jana wakati akitoa maelekezo ya kushughulikia ripoti ya CAG ya mwaka wa fedha 2021/2022 iliyowasilishwa mezani Aprili 6, mwaka huu na Waziri wa Fedha na Mipango.

“Taarifa hizo sasa ziko mikononi mwa Bunge na pia mikononi mwa kamati zinazohusu usimamizi wa fedha za umma ambazo zinaanza kujipanga kuanza kushughulikia taarifa hiyo kikamilifu na kupokea majibu ya serikali kwa hoja zote,” alisema Dk Tulia.

Aliongeza: “Kwa hiyo tusiwe na wasiwasi wabadhirifu wa mali za umma watashughulikiwa ipasavyo kwa taratibu tulizojiwekea.”

Alisema Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) zitawaita wadau kuwahoji na hatimaye kuandaa taarifa itakayowasilishwa bungeni Novemba mwaka huu.

Aliwataka wabunge na wananchi kutoona Novemba ni mbali kwa kile alichosema utawala wa sheria unataka waliotuhumiwa kusikilizwa na wao kuwasilisha taarifa zenye vielelezo ili Bunge liamue kama hoja imeisha na haistahili kufikishwa bungeni kwa ajili ya mjadala.

Aliwaeleza wabunge kuwa baada ya kupokea taarifa ya kamati na maoni na mapendekezo katika kutekeleza jukumu la kuisimamia serikali, wabunge watajadili na hatimaye watatoka na maazimio ya Bunge kuhusu hoja zilizowasilishwa na CAG.

Alisema maazimio hayo yatawasilishwa serikalini kwa utekelezaji ikiwamo kuchukua hatua za kisheria na kinidhamu kwa taasisi na maofisa watakaobainika kujihusisha na matumizi mabaya ya fedha za umma.

“Bunge ni taasisi inayokerwa na kuumizwa zaidi na jambo hilo kwa sababu tunafahamu matarajio ya wananchi kwa serikali na tunafahamu pia Rais Samia Suluhu Hassan anavyohangaika kupata fedha kwa ajili ya ustawi wa wananchi,” alisema Dk Tulia.

Alisema kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, CAG anafanya kazi kwa niaba ya Bunge hivyo maoni na mapendekezo anayotoa na kukubaliwa na Bunge kisha kuwasilishwa serikalini lazima yatekelezwe.

“Katika kutekeleza hili napenda kuwafahamisha wabunge kuwa serikali imewasilisha taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya bunge tuliyoyapitisha mwezi Novemba 2022 kuhusiana na taarifa ya CAG ya mwaka wa fedha 2020/2021 ambayo taarifa imewasilishwa kwangu,” aliwataarifu wabunge.

Habari Zifananazo

Back to top button