Stamico yafungua milango ya uchorongaji Geita

SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limekabidhi mtambo wa uchorongaji kwa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo mkoani Geita (Gerema) ambao umeanza kazi kusaidia upatikanaji wa taarifa sahihi za kijiolojia.

Makabidhiano hayo yamefanyika katika mgodi wa mfano uliopo kata ya Lwamugasa wilayani Geita mkoani hapa lengo likiwa ni kuwasaidia wachimbaji wadogo waachane na uchimbaji wa kubahatisha.

Advertisement

Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, Dk Venance Mwasse amesema mtambo huo ni miongoni mwa mitambo mitano iliyonunuliwa na Stamico ambapo tayari imefanyiwa majaribio na kuonyesha matokeo chanya.

Amebainisha majaribio yaliyofanyika katika migodi ya Nyamongo mkoani Mara, Chunya mkoani Mbeya na migodi iliyopo Dodoma mitambo imechoronga vizuri na mwitikio wa wachimbaji wadogo ni mkubwa.

Ameeleza mtambo wa uchorongaji utaondoa tatizo la kuchimba bila taarifa sahihi za kijiolojia, hali ambayo ilikuwa inapelekea kupoteza mtaji , kutokuaminika na taasisi za kifedha na matumizi ya imani potofu.

“Shirika la madini la Taifa limejipanga ifikapo Aprili 2024 tayari itaingia mitambo mingine mitano na ifikapo mwisho wa mwaka huu wa fedha ambao ni Juni itakuja tena mingine mitano jumla itakuwa 15.

“Lengo ni kuwasaidia wachimbaji wadogo kuweza kugundua zaidi na kuweza kuwa na uhakika ya nini wanakitaka na kipo wapi ambapo itapunguza upotevu mitaji na kufanya waaminike na taasisi za fedha.

“Pia bado kuna changamoto ya utafiti wa awali ambao utawezesha hiki tunachokifanya kifanikiwe, hilo tunalichukua kwa sababu ni suala la kitalaamu, tukilikwepa hilo hizi mashine hazitafanya kazi.” Amesema.

Meneja Uwezeshaji Uchimbaji Mdogo wa Stamico, Tuna Bandoma amesema tayari shirika hilo limeshafudisha wajiolojia waendeshaji wa mitambo hiyo ifanye kazi kwa ufanisi na kwa muda mrefu.

Mwenyekiti wa Gerema, Christopher Kadeo amekiri ujio wa mtambo wa uchorongaji ni mkombozi kwao kwani wataenda kuwa na uhakika wa maeneo wanayochimba na hivo kuinua uzalishaji wa madini.

 

Kadeo ameiomba serikali kuambatanisha ujio wa mitambo hiyo na upanuzi wa maabara ya madini mkoani Geita ili kutoa fursa ya wachimbaji wengi kupata taarifa za uhakika za kijiolojia ndani ya muda mfupi.

Kaimu Mkuu wa mkoa wa Geita, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Cornel Magembe amewasisitiza wachimbaji wadogo kukacha imani za kishirikina na kujikita zaidi katika matumizi ya teknolojia hiyo ya uchorongaji.