Stamico yasaini mkataba mnono na GGML

KAMPUNI ya Madini ya Taifa (STAMICO), imesaini mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Sh bilioni 55.2 na Kampuni ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) mahususi kwa ajili ya shughuli za kuchoronga.

Akizungumuza katika hafla ya kusaini mkataba Machi 27, 2023 mjini Geita, Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, Dk Venance Mwasse, alisema mkataba huo ni matokeo ya ufanisi na kuimarika kwa Stamico.

Amesema Stamico watawajibika kuchoronga mita 95,000 ndani ya mgodi wa GGML,  ambapo awali walikuwa na mkataba wa muda mfupi lakini mkataba uliosainiwa ni wa muda mrefu na thamani kubwa kuwahi kutokea.

“Sisi tumejiandaa vizuri na mtaona tuna mitambo ya kutosha, mpaka sasa tuna mitambo 14 (ya kuchorongea), lakini tutaongeza mingine miwili na itafikia 16.

“Huo ndio mwelekeo wa shirika kuhakikisha kwamba tunaendelea kupata kandarasi kubwa hapa  nchini, na kuweza kutengeneza ajira kwa vijana wenzetu lakini kuwa chanzo cha mapato.

“Mkataba huu tutatekeleza kwa umakini na bila kuleta malalamiko yoyote, na tunaamini utekelezaji wa mkataba huu utapelekea kupata mkataba mkubwa zaidi wa mabilioni mengi zaidi,” amesema.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa GGML, Damon Elder amesema wameingia mkataba na Stamico, kwani wana imani na kampuni hiyo ya kitanzania na watahakikisha wanaendeleza ushirikiano.

Waziri wa Madini Dk Dotto Biteko amesema mkataba huo ni matunda ya uwekezaji uliofanywa na serikali kuhakikisha kampuni ya Stamico inaimarika na kuweza kujiendesha kwa faida.

Amesema hayo pia ni matokeo ya marekebisho ya sheria ya madini iliyofanyika mwaka 2017 inayoelekeza mkampuni zote kubwa za madini nchini  kupata huduma muhimu kwa wazawa.

Waziri Dk Biteko amewataka Stamico kuhakikisha wanazingatia mashariti ya mkataba, kufanya kazi kwa ufanisi  na kuachana na tabia chafu zenye kuharibu taswira ya kampuni za wazawa.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x