Stamico yatakiwa kujikita kwenye umeme

WAZIRI wa Madini,Anthony Mavunde amelitaka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kujikita katika kusaidia upatikanaji wa umeme wa uhakika kupitia makaa ya mawe yanayochimbwa katika Mgodi wa Kiwira – Kabulo.
Mgodi huu una hazina ya mashapo ya makaa ya mawe zaidi tani milioni 80 ambayo yakizalishwa kwa wingi ndani ya muda mfupi manufaa yake ni makubwa.
Akizungumza mkoani Mbeya, Mavunde amesema ni dhamira ya Rais,  Samia Suluhu Hassan  kuona nchi  inajitosheleza kwa nishati ya umeme.
“Hivyo, naiagiza STAMICO iende kuharakisha makubaliano mliyoingia na TANESCO na kukamilisha zile hatua muhimu za awali ili muanze mradi wa kuzalisha Megawati 200 za umeme kutoka kwenye makaa ya mawe, ” amesema
Aidha, amesema Tanzania imejaaliwa rasilimali za kutosha na hivyo ni lazima zitumike kwa maendeleo  kama ambavyo makaa ya mawe hayo yanavyoweza kutumika kama chanzo cha nishati badala ya kutegemea chanzo kimoja (_energy mix_).

Habari Zifananazo

Back to top button