TIMU ya soka ya taifa, Taifa Stars jana ilimaliza safari yake ya kuwania kufuzu michuano ya Mabingwa wa Mataifa ya Afrika ‘Chan’ baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Uganda.
Mechi hiyo iliyochezwa Kampala, inafanya Stars kuaga michuano hiyo kwa jumla ya mabao 4-0 baada ya kufungwa bao 1-0 nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa wiki iliyopita.
Matokeo hayo yanaifanya Uganda kufuzu fainali hizo za wachezaji wa ndani zitakazofanyika Algeria mwakani.
Kikosi cha Stars kilicho chini ya kocha mpya, Honour Janza jana kiliruhusu nyavu zake kutikiswa kwa mkwaju wa penalti dakika ya 14 kupitia kwa Moses Waiswa baada ya Rogers Mato kuchezewa hovyo kwenye eneo la hatari.
Uganda iliandika bao la pili dakika ya 55, mpira uliowekwa nyavuni na Richard Basangwa akiunganisha kwa kichwa krosi iliyopigwa na Waiswa.
Timu hiyo ilihitimisha hesabu zake katika mechi hiyo kwenye Uwanja wa St. Mary’s, Kampala baada ya Mato kufunga bao la tatu dakika ya 75, akiunganisha kwa kichwa mpira wa krosi na kuwaacha mabeki na kipa Aishi Manula wasijue la kufanya.
Kiujumla mechi hiyo ilionekana kuwa upande wa Uganda licha ya Stars kujitutumua mara kadhaa kulishambulia lango la wapinzani wao lakini mipango yao mingi iliishia njiani.
Ni kama vile ilivyokuwa kwenye dakika ya 40, Danny Lyanga aliposhindwa kutumia vyema pasi aliyopewa na John Bocco kwenye eneo la hatari ambapo naye aliishia kutoa pasi fupi iliyoshindwa kumfikia mlengwa na mpira kuokolewa na mabeki wa Uganda.
Ilibaki kidogo dakika ya 62 Stars iandike bao kupitia kwa Lyanga aliyeunganisha kwa shuti mpira uliokuwa ukielea elea langoni mwa Uganda lakini ukazuiliwa na Kibu Denis.
Kiungo Feisal Salum alipambana kuipatia bao Stars lakini jitihada zake hazikuzaa matunda kutokana na mashuti yake kwenda nje ya lango kama ilivyokuwa kwenye dakika ya 69 ya mchezo huo uliokuwa na matumizi makubwa ya nguvu.
Aidha, Stars sasa inajipanga kwa ajili ya kuwania kufuzu michuano mingine ya Afcon ambapo watakutana na Uganda kwenye mechi mbili mfululizo za Kundi F zinazotarajiwa kupigwa Machi 23 na 28, mwakani.