Stars inaweza kufuzu kama itapambana

TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, leo inashuka kwenye Uwanja wa St Mary’s Katende jijini Kampala nchini Uganda kucheza na The Cranes katika mchezo wa kusaka nafasi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan).

Stars katika mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili iliyopita ilipoteza kwa bao 1-0 na kimahesabu kama imejiweka katika nafasi ngumu ya kufuzu.

Hata hivyo, pamoja na kuonekana kama iko katika hatari ya kutolewa, lakini bado Taifa Stars inaweza kushinda na kufuzu kwa mara ya tatu kucheza fainali hizo za Chan kama watapambana.

Stars wasiingie kinyonge katika mchezo huo na wanachotakiwa kulishambulia kwa muda wote lango la wapinzani wao licha ya kucheza ugenini.

Lolote linaweza kutokea, ikiwemo hata kushinda kwa idadi yoyote ya mabao, kwani katika soka unaweza kufungwa hata ukiwa nyumbani kwako kama Stars ilivyofungwa.

Yote kwa yote, Taifa Stars ijue kuwa Watanzania wako nyuma yao na wanaitegemea sana kuiona ikiifunga Uganda na kufuzu kwa fainali hizo za Chan, ambazo tulifuzu kwa mara ya kwanza mwaka 2009 nchini Ivory Coast na 2021 Cameroon.

Chan tumeshiriki fainali zake mara mbili sawa na Afcon ambayo tulicheza mwaka 1980 Nigeria na 2019 Misri, hivyo tunahitaji kuvunja rekodi kwa kufuzu kwa mara ya tatu fainali za Chan ambazo zitafanyika Algeria mwakani.

Hii ni hatua ya pili kwa Taifa Stars katika mbio za kusaka kufuzu kwa fainali za Chan 2023 zitakazofanyika nchini Algeria kuanzia Januari 8 hadi Februari 5. Hizi ni fainali za saba za mashindano hayo.

Katika hatua ya kwanza, Tanzania ilifanikiwa kuiondoa Somalia na kupata nafasi ya kucheza dhidi ya Uganda ili kupata timu itakayokwenda Algeria katika fainali hizo.

Kikosi cha Taifa Stas kwa sasa kiko chini ya kocha mpya, Mzambia Hanoor Janza aliyekuwa akiifundisha Namungo ya mkoani Lindi.

Ni matarajio ya wengi kuwa pamoja na Taifa Stars kuwa chini ya benchi jipya la ufundi, lakini inaweza kufanya maajabu na kuifunga Uganda na hatimaye kufuzu kwa fainali zijazo za Chan 2023.

Hii ni mara ya nne kwa Taifa Stars na Uganda kukutana katika mechi za kufuzu na The Cranes imeshinda mara mbili na Stars mara moja katika mashindano hayo ya Chan.

Katika Chan, Tanzania iliifunga Uganda mabao 3-1 katika mchezo wa kufuzu kwa fainali za mwaka 2009 na The Cranes waliifunga Taifa Stars kwa mabao 4-1 kabla ya Jumapili iliyopita Stars kufungwa 1-0.

Tunaitakia kila la heri Taifa Stars pamoja na kuwa na benchi jipya la ufundi, lakini isikate tamaa ipambane hadi kuhakikisha inashinda mchezo huo na kufuzu kwa fainali Algeria.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button