Stiko: Ntarudi kwenye muziki nikipata pesa

MMOJA wa wasanii wanaouna kundi la Wanaume Family, Salum Khalid maarufu Stiko ameamua kuweka muziki pembeni kwa muda na kujikita katika shughuli za uandaaji wa filamu.

Stiko amesema muziki kwa sasa unahitaji fedha nyingi katika uwekezaji wake hivyo ameamua kuuacha kwa muda afanye fani nyingine anayoona itamuingizia fedha zitakazokuja kuwekeza katika muziki wake.

“Kwa sasa nimeamua kuonyesha kipaji changu kingine nimeachana na muziki kwa muda hadi nitakapopata fedha za kuwekeza katika muziki na ninaimani fedha hizo nitazipata kupitia filamu,” amesema Stiko.

Ameongeza kwamba muda mrefu ameingia kambini kuandaa tamthilia inayotarajiwa kuachiwa mwishoni mwa januari mwakani 2024 ikiwa imehusisha wasanii wenye majina makubwa wakiwemo wa muziki na uigizaji.

“Januari ndiyo nitaanza kuachia kazi ninazoelekea kuzikamilisha kwa sasa naandaa filamu na tamthilia ambayo ntaiachia mwishoni mwa Januari mwakani na humo kutakuwa na majina makubwa ya wasanii wa filamu na muziki, hapo watu wataona upande mwingine wa kipaji changu katika uandaaji wa filamu, ” ameeleza Stiko aliyewahi kutamba na wimbo ‘Saa Mbovu’ aliowashirikisha Chege na Kr.

Habari Zifananazo

Back to top button