CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeanzisha ushirikiano na taasisi za nchini India, wakiwemo watafiti wabobezi kufanya tafiti za mazao mbalimbali yanayohitajika kwa wingi yakiwemo parachichi ,soya, choroko na maharagwe mabichi (Green beans) ili kuwezesha yawe na ubora kwenye masoko ya nchini India.
Makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa Raphael Chibunda alisema hayo kwa Balozi wa India nchini, Binaya Srikanta Pradhan aliyefanya ziara fupi chuoni hapo.
Profesa Chibunda alisema kwenye ushirikiano na tafiti wabobezi katika mazao unalenga kuona ufanisi wa kuzalisha kwa wingi mazao ya aina mbalimbali yakiwemo parachichi ,soya, choroko ,maharagwe mabichi na njegere ili yazalishwe kwenye ubora zaidi wa mahitaji ya soko.
Uongozi wa chuo hicho na balozi huyo walifanya majadiliano ya kukubaliana na kuweka ushirikiano na taasisi za nchini India ikiwemo taasisi ya Teknolojia India (ITI).
Profesa Chibunda alisema serikali ya India na mkampuni ya kutoka nchi humo ni wanunuzi wa mazao mengi ya aina mbalimbali yakiwemo ya viungo kutoka nchini Tanzania.
Alisema kupitia ubalozi wa nchi hiyo, SUA imeingia makubaliano ya ushirikiano na taasisi za nchini India kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo na kuwafundisha wakulima wa Kitanzania njia bora za kilimo cha mazao ambayo yataleta tija kwa nchi hiyo.
Profesa Chibunda alisema lengo ni kuwapa wakulima uelewa wa kujua jinsi ya kuhifadhi mazao ili yanapofika kwenye soko la India yasikumbane na vikwazo vya upungufu wa ubora.
Pia alisema ushirikiano huo utagusa maeneo mengine yakiwemo ya tafiti zinazohusu matatizo yanayokabili nchi hizo na makampuni ya kibiashara, kupeleka wanataaluma na wafanyakazi kwenye mafunzo katika vyuo vikuu vya India ili kupata utatuzi wa changamoto zinazozikabili nchi hizo na watu wake.
Profesa Chibunda alisema chuo hicho pia kimeamua kutilia mkazo suala la teknolojia hasa katika mifumo ya TEHAMA ambapo Tanzania inapaswa kuiangalia nchi ya India kama ni sehemu inayofanya vizuri kwenye eneo hilo.
Alisema Chuo hicho kimeamua kwenda kujifunza kwao badala ya kutumia mifumo ya kununua au kupewa kutoka India pamoja na kuweka mkazo kwenye teknolojia rahisi kwa ajili ya wakulima wadogo.
Katika hatua nyingine alisema chuo Kikuu hicho kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi kinaweza kuwa wenyeji kwa makampuni yanayotaka kuja kufanya maonesho ya zana za kilimo, na chuo hicho kuwa mabalozi wa zana za kilimo kwa Watanzania.
“ Chuo chetu kitatumia hiyo nafasi kuweza kujifunza jinsi ya kutengeneza zana rahisi hasa kipindi hiki ambapo tumeimarisha karakana yetu ya Uhandisi Kilimo”, alisema Profesa Chibunda
Profesa Chibunda alisema chuo kitakuwa na program za pamoja katika upande wa wajasiliamali ili kuzalisha wahitimu watakaoweza kujiajiri na kufanya biashara kwa kuzalisha vitu mbalimbali .
“ Programu hizi zitaepusha changamoto ya wengine kutomaliza mafunzo yao kutokana na sababu mbalimbali na kwa kuzingatia mkakati wa maendeleo kwa miaka mitano ijayo ni cha kuzalisha watu wanaoenda kutengeneza kazi” alisema Profesa Chibunda.