MENEJIMENTI ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kimeshauriwa kuboresha mitaala ili iwe ni kichocheo cha kuzalisha wahitimu wenye ubora watakaoendana na soko la ajira hasa viwandani.
Rai hiyo imetolewa na Wajumbe wa Kamati ya Ushauri wa Viwanda iliyokutana katika mwendelezo wa vikao vyake vya kiutendaji kuendeleza mijadala mbalimbali ikiwa ni Utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).
Kamati hiyo ilijadili namna ambavyo SUA itaweza kuzalisha wahitimu wenye ubora watakaoendana na soko la ajira katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji ikiwemo viwandani.
Msimamizi wa Kamati ya Ushauri wa Viwanda kutoka Chuo Kikuu SUA, Dk Felix Nandonde amesema hayo katika kikao kilichohudhuriwa na wajumbe kutoka SUA na na wengine kutoka taasisi binafsi .
Wajumbe hao wamepitia mitaala na kuchangia mambo mbalimbali ikiwemo mahitaji ya sasa hasa kwenye Sekta ya viwanda ili kuweza kuleta mabadiliko ya kiuchumi kupitia mradi wa HEET.
Dk Nandonde amesema kuwa , kamati hiyo ina jukumu la kushauri chuo katika namna bora ya kupata nafasi ya kujifunza kwa vitendo kwa wanafunzi wanaondelea na masomo yao chuoni hapo ili waweze kuongeza ujuzi na maarifa.
Msimamizi wa Kamati hiyo amesema , lengo ni kuwawezesha kushindana katika soko la ajira pamoja na katika utengenezaji wa nafasi za ajira wao wenyewe.
“Kamati hii ina jukumu la kutoa ushauri kwa Chuo juu ya namna bora ya kupata nafasi ya kujifunza kwa vitendo katika Sekta Binafsi na za Umma kwa wanafunzi waoendelea na masomo chuoni hapa” amesema Dk Nandonde
“ Lengo ni kuwajengea uwezo wa kujiamini, kushindana katika soko la ajira lakini pia kuwa na uwezo wa kutengeneza ajira wao wenyewe”, amesisitiza Dk Nandonde.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati hiyo, Abubakar Nassoro Rizwani kutoka Kampuni ya LAKE GROUP LTD amesema kazi kubwa itakayofanywa na Kamati anayoiongoza ni kukiunganisha Chuo na Viwanda kwa kuainisha mapungufu yaliyopo kwa wahitimu na mahitaji ya waajiri katika soko la ajira nchini.
Katika kikao hicho taasisi binafsi ziliwakilishwa na Kampuni za Bakhresa Food Products, LAKE GROUPS pamoja na Kampuni ya Sahara Ventures zote zikiwa na makao makuu yake jijini Dar es Salaam.