SUA yaeleza mafanikio miaka mitatu ya Samia

CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimepata mafanikio makubwa kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita baada ya kutengewa fedha Sh bilioni 73.6 za utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Raphael Chibunda amesema hayo juu ya mafanikio ya chuo hicho katika kipindi cha uongozi wa miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Profesa Chibunda amesema ,serikali ya awamu ya sita ilifanya maamuzi makubwa ya kutafuta fedha kwa ajili utekelezaji wa kuvipanua na kuviboresha vyuo vikuu vya nchini kupitia mradi HEET na SUA ni sehemu ya wanufaika kwa kutengewa kiasi cha fedha hizo.
Amesema mradi huo ni wa muda wa miaka mitano ambao ulianza kutekelezwa mwaka 2021/ 2022 na unatarajia kumalizikia kwa mwaka 2025 /2026, lengo lake ni kuongeza udahili wa wanafunzi na kuboresha ubora wa elimu ya juu nchini .
Profesa Chibunda amesema kati ya fedha wazizotengewa Sh bilioni 50 ni kwa ajili ya upanuzi wa miundombinu Kampasi za Morogoro ambazo ni Solomon Mahlangu na kampasi kuu ya Edward Moringe, na kiasi cha Sh bilioni 20 zitatumika ni kwa upanuzi wa kampasi ya Mizengo Pinda , iliyopo mkoani Katavi.
“Fedha hizio tumezitenga kwa ajili ya ujenzi wa majengo yakiwemo mabweni mawili moja ni katika kampasi ya Solomon Mahlangu na lingine kwenye kampasi mpya iliyopo mkoani Katavi ambayo ni kampasi ya Mizengo Pinda< “ amesema Profesa Chibunda
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu amesema fedha hizo pia zitatumika kujenga majengo ya ufundishaji matatu ambayo yatajengwa mkoani Katavi , Kampasi ya Solomon Mahlangu na jingine kampasi kuu ya Edward Moringe mkoani Morogoro.
Profesa Chibunda ametaja eneo lingine ni kujenga jengo la dahalia ( Kaftelia) mkoani Katavi , ujenzi mkubwa na upanuzi wa karakana za mafunzo mbalimbali ambazo zilizopo kwenye kampasi zote tatu za Chuo Kikuu cha SUA .
Amesema chini ya mradi huo, chuo kimejenga jengo la maabara mtambuka ambalo linauwezo wa kuchukua wanafunzi 3,200 kwa wakati mmoja kupata mafunzo.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu hicho amesema hatua hiyo imewavutia watu wengi kupenda kusoma katika chuo hicho na kukiwezesha kufanikiwa kuwa na ongezeko udahili wa wanafunzi zaidi ya 3,800 ambao baadhi yao ni wanatoka nje ya nchi.
Profesa Chibunda amesema kumekuwa na ongezeko la wanafunzi tangu serikali ya awamu ya sita imeingia madarakani kutoka wanafunzi 13,0199 na kufikia wanafunzi 17,084.
“Nichukue hii nafasi kuishukuru serikali ya kwamba fedha tuliyoomba tumeshapewa na utekelezaji wa huu mradi ulianza na unaendelea kufanyika,“ amesema Profesa Chibunda.
Amesema mradi wa HEET una malengo mengi na makubwa yapo saba ambapo miongoni mwa hayo ni kupanua miundombinu mbalimbali ya Chuo kikuu hicho.
Profesa Chibunda ametaja eneo lingine ni kusomesha wanataaluma na wafanyakazi ambapo hadi sasa Chuo kimewapeleka masomoni nje ya nchi na ndani ya nchi wanataaluma 62.