SUA yashika namba 42 utafiti Afrika

CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeshika nafasi ya kwanza kitaifa katika nyanja ya utafiti, na nafasi ya 42 katika Bara la Afrika.

Makamu mkuu wa Chuo kikuu hicho, Profesa Raphael Chibunda amesema hayo katika taarifa yake kwa mkuu wa Chuo hicho, Jaji Mstaafu na Waziri mkuu Mstaafu, Joseph Warioba wakati ya mahafali ya 40 ya chuo, yaliyofanyika Novemba 25 , 2022 kambasi kuu ya Edward Moringe mkoani Morogoro.

Kwa mujibu wa Makamu mkuu wa Chuo kikuu hicho kuwa , matokeo hayo yametolewa na google Scholar citation index Mwezi Julai, 2022 .

Profesa Chibunda amesema,katika orodha ya watafiti bora 1,000 Tanzania iliyotolewa na Shirika la ad scientific index , SUA imeendelea kutoa watafiti bora nchini ikiwa na jumla ya watafiti 222.

Amesema kuwa kati ya watafiti bora 100 Tanzania, SUA ilitoa Watafiti Bora 33 na mtafiti bora namba moja nchini anatoka katika Chuo Kikuu hicho.

“Katika nyanja ya taaluma na utafiti Chuo kikuu hiki kimeendelea kufanya vizuri” amesema Profesa Chibunda

Profesa Chibunda amesema licha ya kuendelea kufanya vizuri katika nyanja ya taaluma na utafiti, Chuo kilitumia Sh milioni 458.9 (sh 458,959,843.67 ) kufadhili shughuli za utafiti, machapisho na ubunifu kwa wanataaluma wachanga 34.

Amesema Chuo pia kimepata miradi mipya 25 ya utafiti yenye thamani ya Sh bilioni 8. 075 ( Sh 8,075,789,083) na miradi hiyo inafadhiliwa na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.

Katika Mahafali ya mwaka huu(2022) , jumla ya wahitimu 3,744 (wanaume 2,223 na wanawake 1,479) wametunukiwa Shahada mbalimbali wakiwemo tisa wa Shahada ya Uzamivu.

Habari Zifananazo

Back to top button