SUA yathibitisha ‘mti maziwa’ kutibu magonjwa nyemelezi

MOROGORO: UTAFITI uliofanywa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kilichopo Morogoro umethibitisha mmea ujulikanao kama ‘mti maziwa’ kutibu magonjwa mbalimbali nyemelezi ya ngozi.

Kauli hiyo imetolewa na Mtafiti kutoka Idara ya Tiba ya Wanyama na Afya ya Jamii chuoni hapo, Profesa Robson Mdegela wakati timu kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), ilipofanya ziara chuoni hapo kujionea utafiti uliofadhiliwa na serikali kupitia tume hiyo unavyotoa matokeo chanya kwa jamii.

Serikali imetoa takribani Sh milioni 100 kupitia Costech kwa ajili ya kufanyia utafiti mti dawa huo.

“Tuliutafiti mti huu kwa sababu kati ya masoko ambayo yana vitu vingi vinavyouzika ni vitu vinavyosaidia upande wa ngozi maana yake unaanza kwenye sabuni, kwa kutumia sabuni kinachofuata ni kutumia mafuta ikitokea bahati mbaya kuna ugonjwa wengine fangasi au vidonda kwenye ngozi.

“Kwa hiyo kwa kweli kati ya mifumo inayotumia mazao ya miti dawa kwa wingi acha mfumo wa upumuaji, mfumo wa chakula ni mfumo wa ngozi,” amesema.

Amesema katika utafiti wa mti huo, walitaka kujua usalama wake kwa mlaji, ndipo wakaangalia usalama kwa upande wa vitu vinavyoweza kuguswa na kunusa.

Ameeleza kuwa waliweza kuangalia mwonekano wa mazao ya mti huo, kemikali zilizopo na njia za mikrobailojia na kutambua ni kitu gani kinatakiwa kufanyika.

“Nikimaanisha kuwa huo mti kule ndani unakuwa na viini vya aina mbalimbali, viambata vya aina mbalimbali vipo vinavyotibu na vipo visivyotibu na pia vipo vitakavyofanya ule mmea utumike kama sabuni au mafuta…

“Tulivyopata hivyo viambata tukaviingiza maabara na kutupa matokeo mazuri hivi tunavyoongea tulijitahidi kutengeneza mazao ambayo ni sabuni dawa na losheni,” amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button