SUMAJKT yanunua magari 17 kusaidia uzalishaji mali

MKUU wa Tawi la Utawala Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Brigedia Jenerali Hassan Mabena ameagiza watendaji wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT) kusimamia, kutunza na kutumia vyema magari 17 yaliyonunuliwa ili kuleta tija kwa shirika la uzalishaji mali, jeshi na taifa kwa ujumla kwa lengo la kuongeza mapato.

Brigedia Mabena alikuwa mgeni rasmi uzinduzi wa magari 17 yenye thamani ya Sh bilioni 1.6 yakiwemo ya Makao Makuu ya SUMAJKT, Kampuni ya Ujenzi, Kampuni ya Ulinzi na Kampuni ya Usafi iliyofanyika Dar es Salaam.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Brigedia Mabena alisema magari hayo yakawe chachu kwa kuongeza bidii zaidi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali, hali itakayowezesha kupata faida zaidi na hatimaye kuongeza vitendea kazi vingine.

Alisema azma ya Jeshi la Kujenga Taifa na shirika lake la SUMAJKT ni kuhakikisha kampuni na miradi mbalimbali ya SUMAJKT inakuwa na vitendea kazi vilivyo bora na vya kutosha ili kuweza kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi.

“Nichukue fursa hii kuwataka watendaji wote wa SUMAJKT na JKT kwa ujumla kufanya kazi kwa bidii, weledi na ufanisi ili kuweza kuendana na kasi ya kufikia malengo ya kuanzishwa kwa JKT na shirika,” alisema na kuongeza:

“Tukizingatia haya itasaidia shughuli za uzalishaji mali na utekelezaji wa miradi kufanyika kwa wakati, ubora na kwa tija, jambo ambalo litapelekea shirika kupata miradi mingi na yenye tija.”

Naye Mkurugenzi Mtendaji SUMAJKT, Kanali Petro Ngata alisema ushirikiano uliopo baina ya watendaji wa shirika na wa kampuni tanzu umeleta tija katika biashara na utoaji huduma, kuleta ufanisi katika ukusanyaji wa mapato, udhibiti wa matumizi ya mapato na hatimaye kujenga uwezo wa kuwekeza katika miradi na kuimarisha miundombinu ikiwemo ununuzi wa magari hayo.

Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa SUMAJKT Guard Ltd, Meja Essau Nchimbi alisema kampuni hiyo ina jumla ya magari manne, pikipiki 144, mtambo mmoja na mashine nne zinazotoa huduma kwa wateja katika baadhi ya malindo na miradi.

Habari Zifananazo

Back to top button