Sumaye: Samia anaandaa Tanzania ya kesho – LEAD

WAZIRI Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye amesema Rais Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa ya kuandaa Tanzania ya kesho.

Sumaye alisema hayo jana katika Kata ya Bonga, mkoani Manyara wakati alipopewa nafasi na Rais Samia ya kusalimia wakati msafara wa Rais uliposimama hapo akiwa njiani kwenda Babati.

Rais Samia jana alianza ziara ya kikazi mkoani Manyara.

“Ninashukuru sana Rais kwa kunipa nafasi hii, jana (juzi) nilikuwepo kwenye uchaguzi wa kumpata mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara,” alisema Sumaye na kuongeza:

“Baada tu ya kuchaguliwa nilimwambia lengo la CCM ni kuendelea kuongoza dola na bendera tumekukabidhi wewe Rais Samia uongoze nchi yetu hadi 2025 na tena 2025 hadi 2030, tunasema sio kwa kukupendelea, bali kwa mambo makubwa unayofanya katika nchi yetu.”

Sumaye alisema watu wanaoona mbali wanaelewa anachokifanya Rais Samia kuijenga nchi na Tanzania ya kesho na akaahidi kumsaidia kwa kuwa anachapa kazi kwa kushirikisha Watanzania wote.

Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul alimshukuru Rais Samia kwa namna anavyotumikia taifa na kuleta maendeleo kwa wote.

“Ninakushukuru Rais Samia umenifanya sehemu ya serikali yako na ninapewa ushirikiano na watendaji wake, siwezi kulaumu na kwa unayofanya ya maendeleo kwa wananchi, tutasimama na wewe hadi mwaka 2025,” alisema Gekul.

Alisema Kata ya Bonga ni moja ya kata zilizonufaika na fedha za serikali kwa wananchi wake ambapo imepata shilingi milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa sekondari mpya ya kata na kwa sekta ya elimu kwa ujumla katika eneo hilo zaidi ya Sh milioni 665 zimetolewa.

Aidha, wameahidiwa pia kuongezewa zaidi ya shilingi milioni 100 kuboresha sekta ya elimu huku pia maji, umeme na miundombinu ikiendelea kuboreshwa.

Awali Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alizungumzia hali ya ukame na upatikanaji wa chakula nchini na kusema hakuna Mtanzania atakayekufa kwa njaa kwa sababu serikali imejipanga kufikisha chakula cha bei nafuu katika maeneo yote yenye uhitaji.

Bashe alitoa kauli hiyo baada ya Rais Samia kusimama Kondoa mkoani Dodoma kusalimia wananchi.

Alisema halmashauri nchini zinapeleka taarifa za mwenendo wa bei ya mahindi katika maeneo yao na kwenye maeneo yenye bei kubwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), hupeleka mahindi na kuuza kwa bei nafuu kwa wananchi.

“Tumeshapeleka chakula katika halmashauri 41 zenye uhitaji wa chakula na sisi tunafungua duka chini ya maelekezo ya halmashauri na tunauza chakula kwa mwananchi mmoja mmoja kwa bei ya chini na sio kwa wafanyabiashara,” alisema Bashe.

Alisema pia serikali imetoa ruzuku ya mbolea ili wakulima waweze kumudu gharama na kutumia katika shughuli za kilimo kiweze kuwa na tija.

Aidha, Bashe alisema serikali pia inatoa ruzuku ya mbegu na kuwa miaka mitatu ijayo nchi itakuwa inajitosheleza kwa uzalishaji wa mbegu bora.

Habari Zifananazo

Back to top button