‘Sumu ya nyuki inatibu maumivu ya kichwa, misuli, magonjwa ya ngozi’

‘Sumu ya nyuki inatibu maumivu ya kichwa, misuli, magonjwa ya ngozi’

MTAFITI na mbunifu wa teknolojia ya uvunaji sumu ya nyuki, Patrick Kitosi amesema sumu ya nyuki ina faida nyingi ikiwemo kutibu magonjwa.

Kitosi alitaja magonjwa yanayoweza kutibika kwa sumu hiyo ni kukakamaa kwa misuli, magonjwa ya ngozi na maumivu makali ya viungo na kichwa.

Alisema hayo alipowasilisha mada katika semina ya waandishi wa habari iliyoandaliwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na akasema sumu ya nyuki inafanyiwa utafiti iweze kutibu magonjwa ya saratani na Virusi vya Ukimwi (VVU).

Advertisement

“Nyuki ana mazao mengi kama saba; anazalisha asali, maziwa, nta, sumu na mengine. Vitu anavyozalisha vinatokana na mimea kama maua ya miti na tunajua miti mingine ni tiba,” alisema Kitosi.

Alisema sumu hiyo ina utaalamu wa namna ya kutumia ili kutibu ugonjwa husika mfano kuchanganywa kama kipodozi.

Kitosi alisema katikati ya mkia wa nyuki kuna majimaji ambayo ni sumu yenyewe ambapo ikikusanywa ina matumizi katika sekta ya afya na ili uweze kukusanya alibuni mashine kwa ajili ya kuivuna sumu hiyo.

“Mashine ya kuvuna sumu inayopatikana kutoka kwa nyuki inatumia teknolojia ya elecronc survey kwa sababu ili nyuki aweze kutoa sumu kwanza anatakiwa awe amekasirika hivyo unatafuta namna ya kuwakasirisha waweze kutoa,” alisema na kuongeza:

“Mashine hizi zinatumia umeme hivyo zinakuwa zinazalisha kiwango fulani cha shoti ya umeme na ukiweka sehemu nyuki walipo waweze kufikia na kuigusa wanashtuliwa na shoti, wanakasirika na wanaanza kung’ata mashine,” alisema.

Kitosi alisema wakati wanang’ata, wanaachia hiyo sumu kwa hiyo hivyo wanaachwa kwa muda fulani wang’ate halafu sumu ikusanyike na mashine kutolewa kwani unakusanya sumu kwa kukwangua.

“Mashine inakuwa na sehemu mbili ambayo inazalisha kiwango ya shoti ya umeme na kusafirisha na sehemu ya paneli yenye kioo ya nyuki kung’ata baada ya kung’ata nusu saa unaitoa mashine yako,” alisema.

Kitosi alisema sumu inatoka kwa nyuki kama maji lakini baada ya nusu saa inaganda na ikikwanguliwa kutoka kwenye kioo inakuwa kama unga halafu inapimwa.

Aidha, alisema soko la sumu ya nyuki lipo zaidi katika nchi za India, China, Marekani na nchi nyingine ambazo zinatengeneza dawa.

“Ukivuna unaweza kupata gramu moja hadi tano, wastani wa gharama ya sumu ya nyuki kwa soko la nje ni kuanzia Sh 150,000 mpaka Sh 350,000 kwa gramu moja sehemu zingine hadi Sh 400,000,” alisema Kitosi.

Alisema gharama zinategemea na mimea ambayo nyuki wametumia kwani nyuki wanatofautiana kulingana na mazingira kama nyuki wa Afrika sio sawa na Ulaya.

“Nchi zenye miti mingi sumu yake ni bei ghali kwa sababu nyuki wanapata virutubisho vingi, kundi moja la nyuki linaweza kuwa na nyuki 20,000 hadi 60,000. Wingi wa nyuki unaongeza wingi wa sumu unayopata sumu unavua kwa nusu saa,” alisema Kitosi.

2 comments

Comments are closed.

/* */