Sumu ya panya yadaiwa kuua mwanafunzi Geita

MWANAFUNZI wa kidato cha tatu, shule ya sekondari Nyabubela, mtaa wa Nyakahongolo mjini Geita, Janeth Charles (18), amefariki dunia kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kunywa sumu ya panya.

Mganga wa Zahanati ya Nyakahongolo, Paul Mgini, amethibitisha tukio hilo na kueleza binti huyo alikutwa na umauti Jumatatu Oktoba 24, 2022 majira ya saa kumi jioni wakati akipatiwa matibabu.

“Tulimpokea na kuanza kumhudumia, tukifikiri kwamba kama maelezo ya wazazi yalivyokuwa yakisema anaharisha na kutapika na hivyo tukachukua vipimo, tukidhani ya labda ana tatizo la malaria.

“Lakini vipimo vyote vikaonesha hana malaria, hivyo tulimuwekea dripu ya maji kwa ajili ya kuokoa maisha na wakati tunahangaika kuweka dripu kama nusu saa hivi, hali yake ilizidi kuwa mbaya.

Sehemu ya waombolezaji muda mfupi kabla ya maziko. (Picha zote na Yohana Shida).

“Ndipo yeye mwenyewe akatuambia kwamba amekunywa sumu ya panya, mara baada ya kuongea hayo maneno machache, tulimuuliza kwa nini umekunywa sumu, akakaa kimya hakutujibu. Dakika 15 baadaye, akawa amepatwa na umauti.

“Zahanati yetu haina vipimo vya sumu, hivyo sisi tuliamini kile alichokisema kwamba amekunywa sumu, ambayo ilisababisha kifo chake,” alisema.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyakahongolo, Rubigisa Boaz, amesema kabla ya kupelekwa zahanati, binti huyo  alilalamika maumivu ya tumbo na kisha kuomba apatiwe maziwa na licha ya kupewa hakupata nafuu.

Alisema baada ya msiba huo aliwasiliana na mtendaji wa mtaa, ambaye alitoa taarifa polisi waliofika na daktari wa kituo cha afya Kasamwa na baada ya uchunguzi wakatoa kibali cha mazishi.

Mzazi wa Marehemu, Charles Lugwesa, amesema siku ya tukio binti yake hakwenda shule kwa madai nguo zake alizokuwa amezifua hazikuwa zimekauka, hivyo aliendelea na shughuli za nyumbani.

“Baadaye mama yake akaivisha chakula cha mchana, mtoto akaungana kwenda kula, mtoto baada ya kula tonge mbili tatu hivi akatoka nje, baadaye akarudi akaenda chumbani, akafika akaanguka kitandani,” amesema.  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita hajapatikana kuzungumzia tukio hilo.

 

Habari Zifananazo

Back to top button