Sunak kupiga marufuku sigara Uingereza
LONDON, Septemba 23 – WAZIRI Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak anafikiria kuanzisha hatua zitakazopiga marufuku matumizi ya sigara kwa kizazi kijacho, gazeti la The Guardian liliripoti Ijumaa, likinukuu vyanzo vya serikali.
Kama Sunak atapitisha uwekezekano huo itakuwa ni hatua iliyofanywa na New Zealand mwaka jana ya kupiga marufuku kuuza tumbaku kwa mtu yoyote aliyezaliwa kuanzia mwaka 2009, ripoti hiyo ilisema.
“Tunataka kuhimiza watu wengi zaidi kuacha na kutimiza azma yetu ya kutokuwa na sigara ifikapo 2030, na ndiyo maana tayari tumechukua hatua za kupunguza viwango vya uvutaji sigara,” msemaji wa serikali ya Uingereza alisema katika barua pepe kwa Shirika la Habari la Reuters.
Sera zinazozingatiwa ni sehemu ya msukumo mpya unaolenga watumiaji kutoka kwa timu ya Sunak kabla ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka ujao, ripoti hiyo ilisema.
Mei mwaka huu, Uingereza ilitangaza kuwa itafunga mwanya ambao unaruhusu wauzaji kutoa sampuli za bure za ‘vapes’ kwa watoto kama kizuizi cha sigara za kielektroniki.
Mabaraza ya Uingereza na Wales mnamo Julai yaliitaka serikali kupiga marufuku uuzaji wa ‘vapes’ ifikapo 2024 kwa misingi ya mazingira na afya.