SHIRIKA la Sustaionable Youth Development Partnership (SYDP) limetangaza kuratibu shindano la mbio za marathon zitakazofanyika kwa mara kwanza ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, wilayani Iringa, mwaka huu.
Mbio hizo zilizopewa jina la Great Ruaha Utalii Marathon zinatarajia kufanyika Julai 8, 2023 kwa kushirikisha wakimbiaji zaidi ya 600 wakiwemo watalii kutoka nje ya nchi katika mataifa ya Ulaya, Amerika na kwingineko.
Mratibu wa SYDP ambalo ni shirika linalojishughulisha na utoaji wa elimu ya afya, stadi za maisha na ujasiriamali kwa vijana, na hifadhi na utunzaji wa mazingira, Amim Kilahama aliwakaribisha wadau zikiwemo hoteli zinazotoa huduma ndani na nje ya hifadhi hiyo kujitokeza kudhamini.
“Tunaenda kuandika historia kwa kufanya mashindano haya kwa mara ya kwanza ndani ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha tukilenga kuhamasisha utalii katika hifadhi hiyo na kutunza mazingira yanayotegemewa na hifadhi vikiwemo vyanzo vya maji vya Mto Ruaha Mkuu,” alisema.
Alitaja malengo mengine kuwa ni kusaidia kutangaza fursa za uwekezaji na zilizowekezwa ndani na nje ya hifadhi, ajira zinazoendelea kujitokeza kupitia sekta ya utalii na hifadhi ya mazingira, na ushiriki wa jamii dhidi ya ujangili.
“Mbio hizo zitakuwa za kati ya kilometa 5, 10 na 21 na zitakwenda sambamba na matembezi ya kawaida hifadhini humo ili kuwapa fursa wote watakaojitokeza kujionea vivutio mbalimbali katika hifadhi hiyo,” alisema.
Hifadhi hiyo ya pili kwa ukubwa nchini baada ya hifadhi ya Taifa ya Nyerere ipo kilometa 131 kutoka Iringa Mjini na ni maarufu kwa idadi kubwa ya Tembo wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 10,000.
Hifadhi hiyo ni maarufu pia kwa wanyama aina ya kudu wakubwa na wadogo, pofu, simba, chui, nyati, pundamilia, mbweha, fisi, mbwa mwitu, mamba, viboko, twiga, swala pala, ndege zaidi ya 500 na mimea karibu yote inayopatikana kusini na mashariki mwa Afrika.
Alisema SYDP inaanda mbio hizi huku ikitarajia kupata ushirikiano kutoka Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) kwa kupitia hifadhi hiyo ya Ruaha na wadau wengine zikiwemo hotel mbalimbali zilizopo ndani na nje ya hifadhi.
Alisema kabla ya kufanyika kwa mbio hizo SYDP itaratibu pia ligi ya mpira wa miguu itakayoshiriki timu za vijiji vyote vya tarafa ya Idodi vinavyozunguka hifadhi hiyo ili itumike kufikisha elimu ya malengo ya mbio hizo.
Kilahama alisema hoteli maarufu ya Mabata Makali Lodge and Campsite ni moja kati ya wadhamini wanaotarajia kushirikiana nao kufanikisha mbilio hizo.
Meneja wa Mabata Makali Lodge and Campsite, Nyemo Lekuona alisema; “Tutadhamini mbio hizi kwasababu tunauona mchango wake katika kukuza utalii katika hifadhi hii ambayo sisi ni wadau wake wakubwa tunaotoa huduma za kitalii kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.”
Mbali na kudhamini alisema wanaendelea kujipanga kikamilifu ili kuhakikisha wageni watakaokuja kushiriki mbio hizo wanapata huduma zitakazowawezesha kurudi mara kwa mara katika hifadhi hiyo ili kujionea vivutio vyake.
Mkurugenzi wa Mabata Makali Lodge and Campsite, Eward Athanas alisema; “Hii ni mara ya pili kwa hoteli yetu kudhamini mbio hizo zilizoanza mwaka jana. Tunaomba makampuni na taasisi zingine zituunge mkono kwani mbio hizo zina faida kubwa katika kuindeleza sekta yetu ya utalii.”
Alisema kwa mara ya kwanza mbio hizo za Great Ruaha Utalii Marathon zilifanyika mwaka jana kwa kushirikisha wakimbiaji zaidi ya 100 katika eneo la hotel yake hiyo iliyopo nje ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
“Mwaka huu mbio hizi zinafanyika ndani ya hifadhi na idadi ya wakimbiaji inatarajia kuongezeka na kuzifanya kuwa kubwa zaidi hivyo ni muhimu wadau wengine wakajitokeza kuuinga mkono SYDP ili izifanikishe,” alisema.
Alisema mbio za Great Ruaha Utalii Marathon ni njia mpya ya kutangaza utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwani washiriki wanatarajiwa kuwa mabalozi wazuri wa kuvutia utalii wa hifadhi hiyo.