SERIKALI imeamua kurejesha jukumu la ujenzi wa viwanja vya ndege kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) kutoka kwa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS).
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema hayo bungeni Dodoma akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 na akaomba Bunge liidhinishe bajeti yenye thamani ya Sh trilioni 3.
55.
“Mheshimiwa Spika, kuna suala muhimu ambalo kila mara waheshimiwa wabunge wamekuwa wakilihoji ambalo ni kurejesha jukumu la ujenzi wa viwanja vya ndege kwa TAA kutoka Tanroads. Napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa serikali imechukua maamuzi ya kulirejesha jukumu hilo kwa TAA kama ilivyokuwa awali,” Profesa Mbarawa alilieleza Bunge.
Alisema kwa kuwa jukumu hilo limetekelezwa kwa muda mrefu (tangu 2018) na Tanroads, serikali imeona ni busara na ili kutoathiri utekelezaji wa miradi inayoendelea, baadhi ya miradi ambayo imefikia hatua kubwa ya utekelezaji ikamilishwe na Tanroads na miradi mipya na iliyoanza hivi karibuni (isipokuwa ile inayogharamiwa kwa fedha za wafadhili) itekelezwe na TAA.
“Kwa sasa uchambuzi zaidi unaendelea ili kukamilisha taratibu mbalimbali ikiwemo kufanya marekebisho ya miundo na masuala ya kisheria,” alibainisha Profesa Mbarawa.
Alisema serikali kupitia TAA imeendelea kusimamia shughuli za uendeshaji wa viwanja vya ndege nchini; kuboresha huduma za usalama katika viwanja kwa kutoa huduma kwa ndege, abiria na mizigo ambako hadi kufikia Aprili, 2023 idadi ya abiria 3,237,041 walihudumiwa kupitia viwanja vya ndege vilivyo chini ya TAA sawa na ongezeko la asilimia 35 ikilinganishwa na abiria 2,400,229 waliohudumiwa katika kipindi kama hicho 2021/22.
Aidha, alisema katika kuhakikisha kuwa TAA inaendana na kasi ya ukuaji wa shughuli za usafiri wa anga nchini unaosababisha mahitaji ya upanuzi na ujenzi wa viwanja vipya, imeendelea na juhudi za utwaaji, upimaji na upatikanaji wa hati miliki.
Hadi kufikia Aprili 2023 jumla ya hati miliki 10 za viwanja vya ndege vya Iringa, Chunya, Biharamulo, Morogoro, Kahama, Ifakara, Urambo, Njombe, Lake Manyara na Bukoba zimepatikana.
Profesa Mbarawa alisema TAA imekamilisha ulipaji wa fidia kwa ajili ya utwaaji wa eneo la ziada litakalosimikwa mifumo ya taa za kuongozea ndege katika Kiwanja cha Ndege Dodoma na eneo la upanuzi katika Kiwanja cha Ndege cha Kibondo.
Pia alisema TAA imekamilisha uthamini wa wananchi wanaopisha upanuzi wa Kiwanja cha Ndege JNIA, Simiyu, Kilwa Masoko, Ukerewe na Nachingwea na taratibu za malipo ya fidia kwa wananchi hao zipo katika hatua mbalimbali za kupata idhini. “Vilevile, TAA imeshughulikia mgogoro wa ardhi katika kiwanja cha Mtwara, ambapo imefanya vikao na viongozi wa mkoa na wawakilishi wa wananchi.
Matarajio mwafaka utapatikana kabla ya Julai, 2023,” alisema Profesa Mbarawa.
Akizungumzia kuhusu utaratibu wa urejeshaji wa shughuli za uendeshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) chini ya TAA, alisema wizara kwa kushirikiana na wadau ikiwamo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, imewasilisha serikalini mapendekezo ya kutungwa kwa sheria mahususi ya TAA kwa ajili ya kuwezesha viwanja vyote vya ndege nchini ikiwamo KIA, kuwa chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege.
“Kupitia sheria hii, TAA inaweza kukasimu jukumu la uendeshaji wa kiwanja kwa taasisi nyingine pale ambapo itaonekana inafaa,” alibainisha Profesa Mbarawa.