Taa za Barabara ya Bibi Titi zawaibua watumiaji
DAR ES SALAAM: WATUMIAJI wa Barabara iliyopo katika makutano ya Barabara ya Bibi Titi na Maktaba wameipongeza @habarileo_tz kwa kupelekea taa za barabarani katika makutano hayo kushughulikiwa.
Yapata majuma kadhaa kupitia kipindi cha Habari Kuu kinachorushwa na chaneli ya YouTube ya Daily News Digital wananchi hao waliitaka @habarileo_tz kufikisha kilio chao cha kuharibika kwa taa za barabarani kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA).
Hata hivyo, mamlaka hiyo ilifanyia kazi kero hiyo na hivi sasa tatizo hilo limebaki historia.
Peter Elisha ‘Kanali’ dereva bodaboda amesema iliwachukua takribani miezi mitatu wakitaabika na kukosa muongozo barabarani kutokana na kuharibika kwa taa hizo ila sasa wanafurahia.
“Changamoto iliyobaki ni kuwa taa ‘bulb’ zilizopo zina mwanga hafifu hususani nyakati za mchana,” amesema kanali.
Sauli Mgaya, ni mtumiaji wa barabara hiyo, anasema kwa sasa hawapati usumbufu kuvuka barabarani kwakuwa usalama wao unazingatiwa.
Kwa upande wake, Thomas Sassi anasema taa hizo tangu awali hazikuwa na tatizo ila ni uzembe tu wa kutozifanyia ‘service’ uangalizi wa mara kwa mara.
Naye, ofisa usafirishaji wa jijini Dar es Salaam, Peter Malamsha ameipongeza @habarileo_tz na temesa kwa kurekebisha changamoto hiyo, ingawa anasema mwanga wa taa hizo ni hafifu.