Taarifa ya Mkurugenzi Mkuu TPA hafla utiaji saini uwekezaji bandari
Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
Mhe. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Jaji Mkuu wa Mahakama Tanzania,
Mhe. Katibu Mkuu Kiongozi,
Mhe. Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Mhe. Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu Nchini,
Mhe. Waziri wa Uchukuzi,
Mhe. Mawaziri na Naibu Mawaziri Mliopo,
Mhe. Katibu Mkuu Uchukuzi, Profesa Godius W. Kahyarara
Ndugu Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu,
Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama,
Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemarry Senyamule
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi – TPA, Balozi na Inspekta Jenerali wa Polisi Mstaafu, Mhe. Ernest Mangu,
Timu ya Serikali ya Majadiliano (GNT),
Mwenyekiti wa Group la Kampuni ya DP World na Afisa Mtendaji Mkuu wa DP World,
Wakuu wa Taasisi Mbalimbali za Serikali,
Waheshimiwa Viongozi Waandamizi wa Serikali na Chama,
Menejimenti ya TPA,
Wageni Waalikwa,
Waandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana,
Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Rais,
Kwa niaba ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), naomba niongee machache kuhusiana na tukio hili kubwa na la kihistoria ambalo linaenda kufanya mageuzi makubwa yenye mchango chanya katika huduma za Bandari nchini.
Mhe. Rais,
Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana leo hapa kwa madhumuni ya kushuhudia utiaji saini Mikataba Mitatu ya Uwekezaji na Uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam.
Mhe. Rais,
Naomba kwa namna ya pekee nitoe shukrani zangu za dhati kwako wewe binafsi pamoja na Serikali yako ya Awamu ya Sita unayoiongoza kwa dhamira ya dhati katika kuhakikisha kuwa huduma za Sekta ya Uchukuzi hususani zile za Bandari zinatolewa katika viwango shindani kimataifa kwa kuimarisha uendeshaji wa Bandari zetu. Dhamira hii ya Serikali sasa inaongeza uwezo wa bandari zetu katika utoaji wa huduma kwa ufanisi, kupunguza gharama, kuinua uchumi ikiwa ni pamoja na ukuaji wa uwekezaji, biashara, ajira, mapato ya kodi na yasiyo ya kodi pamoja na kutumia ipasavyo fursa ya kijiografia ya nchi yetu katika kanda ya Afrika Mashariki na Kati kwa ujumla.
Mhe. Rais,
Bandari zetu zinaendeshwa katika hali ya ushindani kama zilivyo bandari nyingine duniani. Mazingira hayo yanachagizwa na mabadiliko ya ukuaji wa sekta ya usafirishaji majini, teknolojia na ukuaji wa uchumi. Hivyo, TPA kama Taasisi iliyokasimishwa jukumu la umiliki, uendeshaji, uendelezaji na usimamizi wa Bandari nchini ina jukumu la kutoa huduma sambamba na kasi ya mabadiliko hayo.
Mhe. Rais
Katika kuendana na kasi ya mabadiliko hayo, moja ya mikakati ambayo imebainishwa katika Mpango Kabambe wa Uendelezaji wa Bandari Tanzania wa mwaka 2009 ambao ulifanyiwa marejeo mwaka 2022, umetoa mapendekezo kwa Serikali kuhusu namna ambayo inaweza kufikia azma yake ya TPA kuwa Mmiliki na/au Mwendelezaji wa bandari nchini na kukasimisha shughuli za uendeshaji kwa Sekta Binafsi ili kuongeza ufanisi wa Bandari za Tanzania.
Mhe. Rais,
Pamoja na kuchukua hatua mbalimbali za maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam, bado ufanisi katika utoaji huduma za bandari haujafikia viwango vinavyotakiwa kimataifa. Hali ya sasa ya utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam imeendelea kuwa ya kiwango cha chini ikilinganishwa na bandari shindani kikanda. Kwa mfano, meli nyingi husubiri nangani kwa muda mrefu kabla ya kuhudumiwa. Leo hii, kuna meli 30 zilozofika bandarini (nangani) zikisubiri kuingia bandarini kushusha mizigo wakati zile zinaazohudumiwa gatini ni jumla la meli 11. Wastani wa meli kusubiri nangani kwa Bandari ya Dar es salaam ni siku 5 ikilinganishwa na siku 1.25 kwa Bandari ya Mombasa na siku 1.6 kwa Bandari ya Durban.
Mhe. Rais,
Ufanisi huu mdogo wa Bandari ya Dar es Salaam umetokana na changamoto mbalimbali zikiwemo: kukosekana kwa mifumo ya kisasa ya TEHAMA ambayo haiwezi kusomana; kutokuwepo kwa maeneo ya kutosha ndani na nje ya bandari kwa ajili ya kuhifadhia shehena ya mizigo pamoja na uchache wa magati au maegesho ya meli; na kukosekana kwa mitambo ya kutosha na ya kisasa ya kuhudumia shehena ambayo teknolojia yake inabadilika mara kwa mara na ina gharama kubwa ya uwekezaji na uendeshaji.
Mhe. Rais
Athari za kutokuwa na ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam ni pamoja na: meli kusubiri muda mrefu nangani ambako kunasababisha kuongezeka kwa gharama ya kutumia bandari ya Dar es Salaam, kwa mfano gharama za meli kusubiri nangani kwa siku moja ni takriban Dola za Marekani 25,000, sawa na takriban Shilingi milioni 58 kwa siku; meli kutumia muda mrefu kupakia na kupakua shehena gatini kwa wastani wa siku 5 ikilinganishwa na siku 1 inayokubalika kimataifa; meli kubwa kutokuja katika bandari ya Dar es Salaam kutokana na kuchukua muda mrefu kuhudumiwa. Hali hii husababisha bandari yetu kuwa bandari inayolishwa shehena na bandari nyingine (feeder port) na hivyo kuongeza gharama ya kutumia bandari hiyo na kuikosesha nchi mapato ambayo yangeweza kutumika katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati nchini ambayo ingesaidia kukuza uchumi na kuboresha huduma za wananchi.
Mhe. Rais
Pia, hali hii ya kukosekana kwa ufanisi inaongeza gharama katika mnyororo mzima wa usafirishaji (total route costs) kutoka nje ya nchi, kupitia katika bandari yetu kwenda nchi za jirani zinazotumia bandari hiyo ya Dar es Salaam. Kwa mfano, gharama ya kusafirisha kasha moja kutoka nje ya nchi (on transit) kwenda nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zinafikia takriban Dola za Marekani 12,000. Hii ni gharama kubwa sana ikilinganishwa na Bandari shindani za Mombasa, Beira, Maputo na Durban ambazo ni wastani wa nusu ambazo zinatumika kwa kutumia bandari ya Dar es Salaam. Gharama za usafirishaji kwa mizigo ya ndani ni takribani Dola za Marekani 6,000 kwa kasha ambazo zinapelekwa kwa mlaji wa mwisho ambaye ni mwananchi wa kawaida. Gharama za kupitisha mzigo kama huo kwa bandari jirani ya Mombasa ni takribani Dola za Marekani kati ya 3,500 hadi 4,000.
Mhe. Rais
Kwa kutambua kuwa Serikali pekee haitaweza kutatua changamoto zilizopo kwenye Bandari ya Dar es Salaam, kuanzia miaka ya 2000, Serikali ilianza kushirikisha sekta binafsi na iliingia mkataba wa upangaji na uendeshaji (lease and concession agreement) na Kampuni ya Kimataifa ya Uendeshaji wa Vitengo vya Makasha, Hutchison ya Hong-Kong China kupitia Kampuni ya TICTS. Mkataba huo ulidumu kwa miaka ishirini na mbili (22) kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2022 na kampuni hiyo ya TICTS ilipewa haki ya kipekee ya kuendesha shughuli za kuhudumia makasha katika gati namba 8 hadi 11 za Bandari ya Dar es Salaam. Wakati huo huo TPA iliendelea kuendesha na kuhudumia maeneo mengine ya Bandari hiyo ya gati namba 0 hadi 7 pamoja na magati ya mafuta ya KOJ na SBM.
Mhe. Rais
Makampuni mengi yamekuwa yakionesha nia ya kuendesha bandari ya Dar es Salaam lakini TPA iliingia makubaliano na Kampuni ya DP World kutokana na uzoefu wake katika uendeshaji wa shughuli za bandari barani Afrika, Asia, Ulaya na Amerika ya Kaskazini na Kusini. Kampuni hiyo pia, ina utaalamu wa kuchagiza mnyororo mzima wa usafirishaji (end to end total logistics chain solution) kutoka maeneo ambayo bidhaa zinatoka mpaka kufika kwa Walaji. Pia, uendeshaji wa maeneo maalum ya kiuchumi (special economic zones) karibu na bandari, usafirishaji baharini na nchi kavu (kupitia njia ya reli), uwekezaji mkubwa katika maeneo mbalimbali ambayo imewekeza pamoja na kuajiri Wazawa katika maeneo hayo.
Mhe. Rais,
Kwa upande wa makampuni mengine ambayo yaliwasilisha mapendekezo yao yalionesha nia ya kuwekeza bandarini pekee na sio kuchagiza mnyororo mzima wa usafirishaji na kutafuta masoko ya kimkakati katika eneo la usafirishaji wa shehena ya mizigo. Pia, baadhi ya makampuni hayo hayana uzoefu wa kuendesha shughuli za bandari barani Afrika wakati Kampuni ya DP World inaendesha takriban bandari sita (6) barani Afrika na bandari zaidi ya 68 duniani kote kwa ufanisi mkubwa.
Mhe. Rais,
Katika kutekeleza mikakati ya Serikali ya kuimarisha shughuli za bandari ya Dar es Salaam; muda mfupi ujao utashuhudia utiaji saini wa mikataba mitatu (3) ya uwekezaji na uendeshaji wa bandari ya Dar es Salaam ambayo ni: Mkataba wa Nchi Mwenyeji, Mikataba ya Ukodishaji na Uendeshaji wa Gati Namba 4 hadi 7 za bandari ya Dar es Salaam. Aidha, Gati Namba 0 hadi 3 za bandari ya Dar es Salaam zitatumiwa kwa pamoja baina ya Kampuni ya DP World na Serikali kupitia TPA kwa ajili ya shughuli zingine za kibiashara na Serikali. Naomba kusisitiza kwamba, mikataba hii haihusishi eneo lote la bandari ya Dar es Salaam na bandari nyingine za Tanzania.
Mhe. Rais,
Naomba kukutaarifu kwamba, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania imeanza mchakato wa kumpata mwekezaji wa ndani au wa nje kwa ajili ya kuendesha Gati Namba 8 hadi 11.
Mhe. Rais,
Katika Mikataba hiyo mitatu (3), Serikali itakuwa ikipokea ada na tozo kutoka kwa Kampuni ya DP World ambazo zitaongeza mapato yake na kupunguza gharama za uendeshaji. Hapo awali, Serikali ilikuwa inatumia takribani asilimia 90 ya mapato yaliyokusanywa katika uendeshaji wa maeneo hayo yaliyokodishwa na kubakiwa na asilimia 10 tu ya mapato yote. Hivyo, kutokana na Mikataba hii, Serikali itaweza kubaki na asilimia 60 ya mapato yote kutokana na gharama zote za uendeshaji kubakia kwa Kampuni ya DP World
Mhe. Rais,
Aidha, faida ya mapato kwa Serikali itokanayo na maboresho ya huduma za bandari kupitia uwekezaji huu itaonekana moja kwa moja kwenye ukusanyaji wa ushuru wa forodha unaokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na Mamlaka nyingine za Serikali zilizopewa majukumu kisheria kukusanya tozo, ushuru na ada mbalimbali kutoka katika shehena zitakazo hudumiwa na Bandari. Ambapo tunatarajia mapato yanayokusanywa na TRA yataongeleka kutoka Shilingi Trilioni 7.8 za mwaka 2021/22 kwa mwaka hadi Shilingi Trilioni 26.7 kwa mwaka ifikapo mwaka 2032/33.
Mhe Rais,
Ushirikishaji wa Sekta Binafsi katika uendeshaji wa Bandari sio kitu kipya kwa Serikali na TPA lakini uwekezaji huu utakaoenda kushuhudia utiaji saini wa Mikataba ni wa aina yake ambao pamoja na masuala mengine ya kitaalam yaliyozingatiwa, umezingatia changamoto ambazo Serikali kupitia TPA ilizipata kupitia uwekezaji uliofanywa na kampuni ya TICTS ambayo muda wa mkataba wake ulikoma tarehe 31 Desemba 2022 pamoja na maoni mbalimbali ya wananchi. Kama nilivyoeleza, uwekezaji huu umezingatia vitu vingi ndani yake kwa maslahi mapana ya nchi ikiwemo:
- Mikataba kuhusisha baadhi ya magati ya Bandari ya Dar es Salaam na sio maeneo yote ya Bandari ya Dar es Salaam na mikataba hii haihusishi bandari nyingine za mwambao na maziwa;
- Mkataba huu una ukomo wa miaka 30 na utakuwa ukirejewa kila baada ya miaka 5 ikiwa ni pamoja na kurejea mpango wa uwekezaji;
- Kutakuwa na kampuni ya uendeshaji ambayo TPA itamiliki hisa;
- Kuwekwa kwa viwango vya utendaji (key performance indicators) ambazo mwekezaji anapaswa kuvifikia;
- Watumishi wa sasa wa TPA wamepewa nafasi ya kuchagua kubaki TPA au kuhamia kwa mwekezaji;
- Jukumu la ulinzi na usalama katika eneo lote la bandari na yaliyokodishwa kwa Kampuni DP World yataendelea kubaki Serikalini;
- Mwekezaji atalipa kodi na tozo zote za Serikali kwa kuzingaia Sheria za Tanzania;
- Sheria za Tanzania zitatumika katika utekelezaji wa Mikataba hii,
- Kutakuwa na fursa za watanzania kushiriki katika uwekezaji huu kupitia vifungu vya Sheria vinavyolinda maudhui ya ndani ya nchi (local contents), na
- Haki ya Serikali kujiondoa katika Mikataba hiyo imezingatiwa.
Mhe. Rais,
Naomba kutumia nafasi hii kuelezea japo kwa ufupi na kwa ujumla manufaa ya uwekezaji huu kwa Serikali na TPA kama ifuatavyo;
- Ongezeko la ufanisi kwa huduma zitakazotolewa kwa meli na shehena hali itakayovutia meli nyingi zaidi na shehena kubwa ya mzigo itakayohudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam,
- Uboreshaji wa huduma za bandari kwa kupunguza muda wa kuchakata nyaraka kwa kutumia mifumo ya kisasa ya TEHAMA ya Bandari itakayofungamanishwa na wadau wote wa Bandari,
- Kuongezeka kwa mapato ya Serikali hususan ya ushuru wa forodha kufuatia ongezeko la shehena na meli pamoja na udhibiti wa udanganyifu kupitia mifumo ya kisasa ya bandari ikakayofungamanishwa na mifumo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
- Kuiongezea uzoefu TPA na kuwajengea uwezo wafanyakazi na watanzania katika uendeshaji wa Bandari kwa viwango vya kimataifa,
- Kuimarisha nafasi ya ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam kikanda na kimataifa;
- Ajira kwa watumishi wa TPA na ajira mpya kwa watanzania kufuatia kupanuka kwa wigo wa shughuli za uendeshaji wa Bandari;
- Kupungua kwa gharama za kusafirisha mizigo kupitia bandari ya Dar es Salaam;
- Kuwepo kwa meli za moja kwa moja kutoka bara la Mashariki ya Kati kuja Tanzania ikilinganishwa na hivi sasa ambapo mizigo ya Tanzania huja kupitia nchi jirani;
- Siku za kusafirisha mizigo kutoka Mashariki ya Kati na Mbali zitapungua kutoka siku 30 za sasa hadi siku zisizozidi 15;
- Kuchochea ukuaji wa Sekta nyingine za Uchukuzi kama vile reli na barabara kufuatia ongezeko la shehena linalotakiwa kusafirishwa kutoka bandarini kwenda sehemu nyingine, na
- Kuchagiza na kuchochea shughuli nyingine za kiuchumi kama vile kilimo, ufugaji, usafirishaji wa madini pamoja na biashara.
Hivyo basi, naomba kutoa rai kwa watanzania kujipanga na kuhakikisha kuwa wanatumia vyema fursa mbalimbali zitakazojitokeza kufuatia uwekezaji huu ikiwemo usafirishaji wa mizigo kutoka Bandarini, vifungashio na vifaa mbalimbali vya kufunga mizigo pamoja na huduma mbalimbali za kuongeza thamani ambazo katika Mikataba ya uwekezaji, Serikali imehakikisha fursa hizi wanapewa wazawa (watanzania).
Mhe. Rais,
Uwekezaji huu wa kihistoria ni mwanzo wa safari ndefu ya uwekezaji wa kimkakati ambao Serikali inategemea kuufanya kama vile uwekezaji katika Kanda Huru za Kiuchumi (Free Economic Zone) katika Bandari Kavu ya Kwala ambapo huduma mbalimbali ikiwemo zile na kuongeza thamani bidhaa za ndani na nje ya nchi na baadae kuzisafirisha kupitia Bandari zetu au njia nyingine yoyote ya usafirishaji. Uwekezaji wa kimkakati unaoendelea kufanywa na TPA, unatarajiwa kutoa suluhisho la changamoto za muda mrefu kwa wakulima, wafugaji na wazalishaji mbalimbali kwa kuwafungulia fursa za uhakika za masoko za kimataifa.
Mhe. Rais,
Menejimenti ya TPA inapenda kutoa shukrani pekee kwako na Mhe. Rais na Serikali yako ya Awamu ya Sita kwa kuelekeza, kusimamia na kuratibu vyema mapinduzi haya ya Sekta ya Uchukuzi. Tunapenda kukuhakikishia kwamba, TPA ipo tayari kusimamia kikamilifu na kwa uzalendo mkubwa utekelezaji wa Mikataba hii ili kuhakiksha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wananchi wote wanaendelea kunufaika na matokeo ya uwekezaji huu wa Bandari ya Dar es Salaam.
Mhe. Rais,
Kwa heshima na taadhima, naomba kuwasilisha.