Taasisi kukwamua wakulima kiuchumi zao la maharage, alizeti
TAASISI ya Kuboresha Mifumo ya Masoko ya Kilimo Nchini (AMDT) imejidhatiti katika kuiunga mkono serikali kuwakwamua wakulima kiuchumi wa maharage na alizeti.
Hatua hiyo ni baada ya kuongeza mapato yao kupitia kilimo cha umwagiliaji nchini.
Wakulima wengi wamekuwa wanajikosesha fursa ya kujipatia kipato mara dufu kupitia kilimo cha umwagiliaji, hasa katika kipindi cha kiangazi, licha ya kuwepo maeneo karibu na mito inayo tiririsha maji katika kipindi chote cha mwaka kando na maeneo yao ya kilimo.
Hayo yalisemwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya AMDT, Charles Ogutu wakati wa ziara yake na waandishi wa habari kutembelea shamba la mfano wa kilimo cha maharage lililopo kijiji cha Londoto kata ya Msitu wa Tembo wilayani Simanjiri mkoani Manayara jana.
Lengo kubwa ni kutoa elimu kwa wakulima wa mazao hayo ili walime misimu miwili katika mwaka na kujiongezea kipato kwa kuuza mazao hayo na kujihakikishia kupata chakula cha uhakika katika kipindi chote cha mwaka mzima.
“Tunaendelea kutoa elimu ya namna bora ya kilimo cha umwagiliaji, kutipia mafunzo ya shamba darasa yanayotolewa na taasisi mbalimbali za utafiti za mbegu bora na kuboresha kilimo cha mazao nchini”.
“Awali wakulima wa zao la maharage walikuwa wakivuna kati ya gunia tatu hadi tano kabla ya kupatiwa mafunzo maalum ya shamba darasa, tofauti na sasa, ambapo wanavuna kati ya gunia nane hadi kumi kwa misimu miwili kwa mwaka, alisema Afisa Kilimo wa Kata hiyo, Charles Ndalechi.
Matokeo hayo chanya yamesababishwa na mwitikio wa wakulima katika kulima kwa kutumia mbegu bora, matumizi sahihi ya viwatilifu na njia sahihi za kilimo cha umwagiliaji baada ya kupatiwa mafunzo na taasisi ya Beula.
Mnufaika wa mafunzo hayo, Fadhili Seif ambaye anajishughulisha na kilimo cha maharage katika kijiji cha Londoto wilayani Simanjiro mkoani Manyara, amekuwa mfano wa kuigwa baada ya kuwa mstari wa mbele katika kilimo cha umwagiliaji hasa katika kipindi hiki kiangazi.
Ameiomba serikali iwasaidie kukabiliana na wadudu waaribifu na magonjwa yanayo dhoofisha mimea kwa kupunguza ghalama za viwatilifu, kwani kwa sasa vinapatikana kwa bei ya juu inayo pelekea kushindwa kumudu kununua dawa hizo za kuulia wadudu hao waaribifu wa mazao yao shambani.