Taasisi ya Kuwait yaiahidi makubwa JKCI

TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imesema Shirika la Children’s Heart Charity Association la Kuwait limeahidi kuboresha tiba za kibingwa katika taasisi hiyo.

Wataalamu wa shirika hilo walitembelea taasisi hiyo jana na kuona watoto wanaotibiwa JKCI. Baada ya kutembelea eneo hilo, walisema wamefarijika kuona uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali kwa ajili ya matibabu ya moyo yanayotolewa hapa nchini kwa Watanzania wenye uhitaji wa huduma hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge alisema shirika hilo limeahidi kuangalia kama kutakuwa na uwezekano wa kujenga jengo jipya la JKCI ambalo litaongeza upatikanaji wa huduma za matibabu na upasuaji wa moyo hususani kwa watoto.

“Katika kushirikiana nasi, wataalamu hawa wameahidi pia kutuletea vifaa tiba ambavyo vitatumika katika matibabu ya watoto ikiwa ni sehemu ya kutoa huduma rafiki kwa watoto kwani watoto wengi wanatoka katika familia zisizokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu,” alisema Dk Kisenge.

Alisema shirika hilo pia limeahidi kushirikiana na JKCI kutoa mafunzo kwa wataalamu kwa kuwaleta wataalamu wao nchini kubadilishana uzoefu na wa JKCI.

“Magonjwa ya moyo kwa watoto yanazidi kuongezeka hapa nchini hivyo kuongeza uhitaji wa matibabu ya magonjwa hayo kuwa kubwa, naamini ujio wa wataalamu hawa kutoka nchini Kuwait utaenda kusaidia watoto wengi kufikiwa na matibabu haya ya moyo,” alisema Dk Kisenge.

Aidha, alisema JKCI katika mpango mkakati wa kutoa huduma bora na rafiki kwa Watanzania, imekuwa ikiwafuata wananchi mahali walipo ili kila mwenye uhitaji na huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo aweze kuzipata.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya JKCI, Profesa William Mahalu alisema wataalamu wa afya kutoka nchini Kuwait wameonesha nia ya kusaidia kutibu watoto wenye magonjwa ya moyo.

Habari Zifananazo

Back to top button