Taasisi ya Mkapa yakabidhi vifaa vya maabara

Taasisi ya Mkapa yakabidhi vifaa vya maabara

TAASISI ya Benjamin William Mkapa imetoa mashine tano za maabara (Semi automatic Biochemistry) kwa uongozi wa Mkoa wa Mtwara kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya katika mkoa huo.

Mashine hizo zenye thamani ya shilingi milioni 50 zimetolewa leo ikiwa taasisi hiyo inaadhimisha miaka 17 tangu kuanzishwa kwake Aprili 13, 2006.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano, Ofisa Miradi Mwandamizi Taasisi ya William Mkapa, Dk David Olemkopi amesema lengo kuu la msaada huo wa mashine ni kuimarisha upatikanaji wa huduma za kimaabara kwenye hospitali na vituo vya Afya mkoa wa Mtwara.

Advertisement

Mashine hizo pia zitasaidia wagonjwa kupewa huduma sahihi za kimatibabu kwa kufanyiwa vipimo sahihi kwa muda mwafaka.

“Mashine hizi zina uwezo wa kufanya vipimo mbalimbali ikiwemo vipimo vya moyo, figo, ini, vichocheo vya mwili (hormones) kwenye damu ya mgonjwa na ina uwezo wa kufanya vipimo zaidi ya 100 Kwa siku,” amesema.

Ofisa huyo amesema Taasisi ya Benjamin William Mkapa kwa kushirikiana na Wilaya husika itaendelea kufanya ufuatuliaji wa utoaji huduma za maabara kwenye vituo ambavyo vimepokea mashine hizo kupima uboreshaji wa huduma za afya kama matokeo ya uwepo wa mashine hizo za maabara.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara, Edina Katalaiya  ameshukuru uongozi wa Taasis ya Benjamin William Mkapa kwa kuwapa mashine hizo, huku akiahidi kuwa mkoa utasimamia na kuhakikisha mashine hizo zinapelekwa na kutumika ipasavyo katika vituo vya Afya vyenye uhitaji.

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *