Taasisi yadhamiria kuinua wanawake Tanzania

TAASISI ya Mke wa Rais wa Zamani wa Afrika Kusini, Graca Machel inakusudia kuwainua wanawake kiuchumi nchini Tanzania baada ya miradi yao kuathiriwa kipindi cha maambukizi ya virusi vya Corona.

Mshauri wa Mradi wa kuwainua wanawake unaosimamiwa na Taasisi hiyo ya Graca Machel, kutoka Taasisi ya New Faces New Voices Tanzania, Judith Sando amesema hayo jijini Dar es Salaam baada ya kukutana na kujadili juu ya mafanikio na changamoto za wanawake wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa hapa nchini.

Sando amesema kipindi hicho cha maambukizi ya virusi vya Corona, wafanyabiashara wanawake wa Tanzania na dunia kwa ujumla walipata changamoto katika biashara zao hivyo kuathirika, nao wale waliokuwa kwenye ajira baadhi yao walipunguzwa kazi.

Advertisement

“Hivyo taasisi hii ipo kwa ajili ya kumsaidia mwanamke aweze kuinuka tena kiuchumi, lakini ki nchi tunaangalia sera za namna gani zimewekwa kwa ajili ya kumsaidia huyu mwanamke kuweza kusogea hatua kwa hatua baada ya maambukizi hayo,” amesema.

Amesema kupitia taasisi hizo zilizopo kwenye mradi huo wanawake watashirikiana na wengine wabobevu kwenye masuala ya fedha ili watoke sehemu moja kwenda nyingine.

Kwa upande wake Meneja wa taasisi hiyo ya New Faces New Voices nchini, Emma Kawawa amesema wanashirikiana na taasisi nyingine zilizopo chini ya Mradi huo wa Graca Machel hapa nchini ili kuwainua wanawake kiuchumi baada ya kuathiriwa na maambukizi ya corona na mengineyo.

Naye Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), ambaye pia ni Mratibu wa Mtandao wa Waandishi wa Habari wa Mfuko huo wa Graca Machel, Dk Rose Reuben amesema ni vizuri waandishi wanawake wakaandika taarifa zinazoendana na wanawake hasa katika huo mradi katika masuala ya fedha.

“ Ni jambo zuri sana ambalo waandishi wa habari wanaweza wakalifanyia kazi kwa sababu wataandika taarifa za kweli na zile zinazohusu wanawake katika masuala ya fedha.

“Baada ya Covid 19 wanawake waliathiriwa kwa namna moja ama nyingine wengine mitaji yao ilikatika lakini wengine mpaka sasa utendaji wao umebadilika, wengine wamelazimika kwenda mitandaoni ambapo ndio njia sahihi ya kuweza kuokoa mitaji yao,” amesema.

Ameongeza kuwa wanawake wengi bado wanafanya shughuli kwa namna ambayo haiwapatii tija kwa sababu ile mifumo ya kibiashara imebadilika, wakati wengine wanauza kimitandao wao wanaendelea kufanya katika eneo lile moja.

/* */