Taasisi yaenzi miaka 101 ya Nyerere
TAASISI ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere leo inafanya kongamano la kumbukizi ya miaka 101 ya Baba wa Taifa, Julius Nyerere.
Akizungumza jijini hapa, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Peter Mavunde alisema kongamano hilo linafanyika kwenye ukumbi wa Chimwaga na mgeni rasmi anatarajia kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Alisema kuwa lengo la kuandaa kongamano hilo ni kurithisha vijana kuhusu yote ambayo Nyerere aliyafanya kwa taifa. “Taasisi iliona mwaka huu iwahusishe vijana wetu, wanafunzi wetu wa vyuo vikuu, vya kati, shule za msingi na sekondari ili taasisi iweze kuianza safari ya kuwarithisha vijana wetu wafuate nyendo za Nyerere, mambo mazuri aliyoliachia taifa hili, amani, lakini muungano unazidi kuimarika,” alisema.
Alisema katika maadhimisho hayo, mbali na kongamano la kumbukizi ya miaka 101 ya kuzaliwa kwa Nyerere pia utafanyika uzinduzi wa klabu za mazingira za Mwalimu JK Nyerere vyuoni na shule za msingi na sekondari kwa lengo la utekelezaji wa kitaifa wa utunzaji wa mazingira endelevu.
Pia kutakuwa na kuzindua mpango maalumu wa urithishaji kwa watoto na vijana mambo mazuri ya Baba wa Taifa aliyoliachia taifa kupitia midahalo, makongamano na semina mbalimbali na usajili wa wanachama.