Taasisi yaja na mbinu ya kuwainua wajasiriamali, wastaafu

Mjasiriamali Mjasiriamali
Mjasiriamali

KATIKA kuwainua kibiashara wajasiriamali wadogo na wa kati pamoja na wastaafu nchini, Taasisi ya Fedha ya Lesthego imekuja na mbinu mpya ya kuwawezesha kupata mikopo kwa urahisi.

Taasisi hiyo ya benki imefungua akaunti maalumu kwa ajili ya wajasiriamali na wastaafu zitakazowawezesha wenye sifa kufungua akaunti kwa Sh 1,000.

Wajasiriamali watakaoguswa na mpango ni pamoja na baba na mamalishe, bodaboda na hata machinga.

Advertisement

Lengo la kuanzisha akaunti hizo ni kumuwezesha kila mjasiriamali kupata huduma za kibenki mahali alipo bila gharama pamoja na mikopo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa akaunti hizo, Mkuu wa Kitengo cha Mauzo katika benki ya Letshego, Leah Phili alielezea akaunti ya mjasiriamali waliyoipa jina la mjasiriamali mpambanaji kuwa inafunguliwa kwa Sh 1,000 na mhusika anaweza kukopa hadi Sh 250,000 kulingana na ukubwa wa biashara yake.

Kwa upande wa akaunti ya wastaafu aliyopewa jina la mstaafu mwenye malengo, anaweza kufungua akaunti hiyo kwa Sh 1,000 na kuruhusiwa kukopa kulingana na kiasi cha pensheni anayopata kila mwezi.

Phili alisema akaunti zitamsaidia mjasiriamali aisiye na nyaraka za biashara kupata huduma za kibenki.

“Tumeona ombwe kwenye eneo hilo ndio maana tumeamua kuwavuta karibu wajasiriamali hasa wanawake. Matarajio yetu sokoni baada ya kupeleka bidhaa hizi ni kufungua akaunti mpya 900 za wajasiriamali ifikapo mwisho wa mwaka huu na akaunti 100 za wastaafu,” alisema.

Meneja Masoko wa Benki ya Letshego, Uswege Mwaipiana alisema benki hiyo yenye matawi nane nchi nzima na mawakala kila mkoa imedhamiria kuwafikiwa watanzania na kuwahudumia kwa viwango vya juu.

“Hapa Dar es Salaam tunayo matawi matatu, tupo Mwanza, Tanga, Mbeya, Dodoma na Arusha lakini pia kila mkoa tunao mawakala wa benki yetu ya Letshego na huduma za kidijitali zinapatikana kupitia mtandao wetu wa kibenki,” amesema Mwaipiana.

Benki ya Letshego ilianza shughuli zake hapa nchini mwaka 2016 ikiendelea kukua na kupanua wigo wa wateja na matawi.